MV MWANZA “HAPA KAZI TU” KUKAMILIKA MWEZI WA TATU 2022

 

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho akipanda ngazi ili kukagua maendeleo ya ujenzi wa meli mpya ya MV. MWANZA “Hapa Kazi Tu”. Meli hiyo inajengwa jijini Mwanza na Kampuni ya GASEntec Shipbuilding Engineering ya Korea Kusini kwa gharama ya Bilioni 89.76, itakapo kamilika itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1200 na mizigo tani 400.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, akiongea na baadhi ya wahandisi wa Tanzania wanaoshiriki ujenzi wa meli mpya ya MV MWANZA “Hapa Kazi Tu” jijini Mwanza.. Kutoka kushoto ni Mhandisi Moses Malambuka, Mhandisi Mwanaisha Ally na Mhandisi Majid Ilunga.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho akitoa maelekezo kwa Wataalamu wanaojenga meli mpya ya MV. MWANZA “Hapa Kazi Tu”, alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Meli hiyo inayojengwa jijini Mwanza. Kushoto kwa Waziri ni Rasmus Bayer (Naval Architect), pamoja na wataalamu wengine kutoka Kampuni ya GASEnteac Shipbuilding Engineering, inayojenga meli hiyo.

Wataalamu wa teknolojia ya kisasa ya ujenzi wa meli kutoka Kampuni ya GASEntec Shipbuilding Engineering, inayo jenga meli mpya ya MV MWANZA “Hapa Kazi Tu”, jijini Mwanza, wakiendelea na usimikaji wa mifumo ya mabomba kwenye meli. Meli hiyo inajengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 89.76 na inatarajiwa kukamilika mwezi wa tatu mwaka 2022.

Muonekano wa maendeleo ya ujenzi wa meli mpya ya MV MWANZA “Hapa Kazi Tu” inayojengwa jijini Mwanza na Kampuni ya GASEntec Shipbuilding Engineering kwa gharama ya Shilingi Bilioni 89.76. Ujenzi wa meli hiyo unatarajiwa kukamilika mwezi wa tatu mwaka 2022 na itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1200 na mizigo tani 400

……………………………………………………………………………………………..

Imeelezwa kuwa ujenzi wa meli mpya ya MV MWANZA “Hapa Kazi Tu” inayojengwa katika ziwa Victoria jijini Mwanza, na Kampuni ya GASEntec Shipbuilding Engineering ya Korea Kusini, kwa gharama ya shilingi Bilioni 89. 76, unatarajiwa kukamilika mwezi wa tatu mwaka 2022.

Akikagua maendeleo ya ujenzi wa meli hiyo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, amewaeleza waandishi wa habari kuwa, ujenzi wa meli hiyo sasa umefikia asilimia 39.3 na kwamba itakapo fika mwezi wa kumi mwaka huu,  itashushwa kwenye maji kwa ajili ya kuendelea na kazi zitakazokuwa zimebaki ikiwa ni pamoja na kufanya majaribio ya mifumo ya uendeshaji wake.

“Nimefurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa meli hii, na cha kufurahisha zaidi MV MWANZA “Hapa Kazi Tu” inajengwa vijana wa kitanzania 150 waliobobea katika fani ya Uhandisi na wanasimamiwa na Wakorea 14 tu. Hii ina maana kuwa katika miradi mingine ya ujenzi wa meli kutakuwa na vijana wa kitanzania wenye uzoefu na utaalamu wa kutosha katika teknolojia hii ya ujenzi wa meli za kisasa”

Aliongeza kuwa ujenzi wa meli mpya ya MV MWANZA “Hapa Kazi Tu” umetoa fursa kwa wanafuzi wa kitanzania kufanya mafunzo kwa vitendo, ambapo hadi sasa mradi wa ujenzi wa meli mpya ya MV MWANZA tayari una wanafuzi 25 wanaofanya mafunzo ya ujenzi wa meli kwa vitendo.

Nae Rasmus Bayer (Naval Architect) kutoka Kampuni ya GASEntec Shipbuilding Engineering inayojenga meli hiyo ameeleza kuwa, ujenzi wa meli hiyo sasa umefikia hatua ya usimikaji mifumo ya mabomba ya mafuta, maji safi na maji taka pamoja na uunganishaji wa bodi ya meli na kwamba itakapo kamilika itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1200 pamoja na mizigo tani 400.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Eric Hamissi, amewaambia waandishi wa habari kuwa Kampuni yake ina jumla ya meli 14, kati ya hizo meli tisa ziko katika ziwa Victoria, meli tatu ziko ziwa Tanganyika na meli mbili ziko ziwa Nyasa. Bwana Eric aimeishukuru Serikali pamoja na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kazi kubwa inayoendelea ambayo imepelekea kuungwa mkono kwa sera ya nchi ya kutoa ajira kwa vijana.

Waziri Chamuriho alikuwa Mkoani Mwanza akitokea Kigoma kwa ajili ya kuzindua Baraza la Wafanyakazi wa MSCL pamoja na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Meli mpya ya MV MWANZA “Hapa Kazi Tu”.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Post a Comment

Previous Post Next Post