………………………………………………………………………………………
Na Grace Semfuko, MAELEZO
Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imewataka Wanawake nchini kuchangamkia fursa za uwekezaji katika sekta hiyo, ili kuinua pato lao na familia huku wakiliingizia Taifa fedha za kigeni kupitia Watalii wa ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Bi. Devotha Mdachi amesema mchango wa Wanawake katika sekta ya utalii unahitajika kwa kiwango kikubwa kutokana na wingi wa kundi hilo nchini, na iwapo watawekeza kwa kasi wataweza kuongeza tija katika sekta hiyo.
Aliyasema hayo wakati akizungumza na Jumuiya ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TABWA) walipokuwa safarini kuelekea katika hifadhi ya Taifa ya Saadani kuangalia fursa na vivutio vya utalii kwenye hifadhi hiyo ya kipekee Afrika Mashariki.
“Sekta hii imekuwa ikitoa ajira kwa Wanawake wengi sana hapa Tanzania, sisi Bodi ya Utalii tumetambua hilo na tunataka kuwaonesha kwamba wanao uwezo wa kumiliki kampuni, kuendesha biashara za utalii na ushika nafasi za uongozi katika sekta a utalii, kuna umuhimu mkubwa wa kumuenzi mwanamke kwa sababu tunajua ndio nguzo ya familia, kupitia Wanawake tunaamini wataweza kuhamasisha Familia zao kwenda kutalii” alisema Bi. Mdachi.
Aliyataja maeneo ambayo Wanawake wanaweza kuwekeza katika Sekta ya Utalii kuwa ni pamoja na ujenzi wa hoteli za kisasa za kitalii, uuzaji wa bidhaa za urembo za asili ya Mtanzania, mapishi ya chakula cha asili, kuanzisha makampuni ya kutembeza watalii na shughuli nyinginezo nyingi.
Nae Mkurugenzi wa ya Jumuia ya wanawake Wafanyabishara Tanzania (TABWA) Bi Noreen Mawalla amesema jumuiya hiyo imeamua kuunga mkono juhudi za Serikali, za kuinua uchumi wa Wanawake kupitia biashara mbalimbali hivyo eneo la Utalii wameliona ni eneo la kipekee ambalo wanawake wengi wanaweza kuwekeza.
“Sisi TABWA kwa kipekee kabisa naomba nikuhakikishie kwamba tumeziona fursa katika eneo hili la utalii, Wanawake tutawekeza huko kwa sababu nia tunayo, uwezo tunao na nguvu tunazo, sisi tunaangalia fursa na kuzinadi kwa wanachama wengine ambao wana uwezo kwenye uwekezaji huu” amesema Bi. Mawalla.
Jumuiya ya Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TABWA), ilifanya maonesho ya wafanyabiashara katika viwanja vya Mlimani City Jijini Dar es Salaam, ambapo pia walitembelea hifadhi ya Saadani lengo likiwa ni kutalii na kuangalia fursa za Uwekezaji kwenye eneo hilo.
Mwisho