KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA UJENZI BRT II MBAGALA -Yaipongeza TANROADS kwa kazi nzuri

 

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale( wa nne kutoka kulia), akiikaribisha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu inayoongozwa na Mwenyekiti Mhe. Selemani Kakoso (wa tatu kutoka kulia) ilipotembelea Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya mabasi yaendayo kasi (BRT) kwa awamu ya pili leo Machi 16, 2021, barabara hiyo inaanzia Kariakoo hadi Mbagala Jijini Dar es Salaam.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imekagua Mradi wa Ujenzi wa Barabara za mabasi yaendayo haraka kwa awamu ya pili unaoanzia Kariakoo hadi Mbagala Jijini Dar es Salaam.
Kamati hiyo imeipongeza TANROADS chini ya Mtendaji Mkuu Mhandisi Patrick Mfugale na kuitaka kusimamia vyema ujenzi wa mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati uliopangwa na kwa kiwango kinachotakiwa.    

Muonekano wa Kituo cha mabasi yaendayo kasi (BRT awamu ya pili kilichopo katika Eneo la Kariakoo Jijini Dar es Salaam ambapo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 78, Kituo hicho kitatumika na abiria wanaotoka Kariakoo kuelekea mbagala baada ya ujenzi wa Barabara ya BRT awamu ya pili ya Kariakoo hadi Mbagala Jiji Dar es Salaam Kukamilika.

**************************************

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Seleman Kakoso amepongeza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), kwa kazi nzuri ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Mabasi ya Mwendo Haraka (BRT).

Mheshimiwa Kakoso amesema TANROADS wameaminiwa kwani kimsingi mradi huo ulikuwa utekelezwe na Halmashauri, huku akiwataka kuukamilisha kama mkataba unavyoelekeza pamoja na kwamba kulikuwa na changamoto ya Covid-19.

“Tunawapongeza sana TANROADS, mmeaminiwa, kimsingi huu mradi ulitakiwa kutekelezwa na Halmashauri,” amesema Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Miundombinu, Seleman Kakoso.

Mwenyekiti huyo amesema ameiagiza Serikali inapooingia kwenye miradi kama hii kuhakikisha wanaisimamia vizuri. Amepongeza TANROADS kwa kuwalipa fedha stahiki za maeneo yao zaidi ya shilingi bilioni 34.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema mradi huo ni wa awamu ya pili unaohusisha ujenzi wa barabara kilomita 20.3, madaraja ya juu (flyover) mbili na vituo vya mabasi.

Amesema mradi huo utaanzia katikati ya Jiji hadi Mbagala utakaogharimu fedha za Marekani 159,320,563.

Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Patrick Mafugale, amesema ujenzi wa stesheni kuu ya BRT Mbagala umefikia asilimia 77, ambapo kufikia Julai mwaka huu itakuwa imekamilika.

Ujenzi wa stesheni kuu ya BRT Mbagala kwa sasa umefikia asilimia 77 na kufikia Julai kituo kitakuwa kimekamilika,” amesema Mtandaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mfugale.

“Kazi za ujenzi zimegawanywa katika sehemu mbili, ujenzi wa barabara kilomita 20.3, flyover mbili, vituo vya mabasi 27, daraja moja la juu la waenda kwa miguu eneo la Mbagala na daraja moja la juu la reli eneo la BP,” amesema Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mfugale.

Mtendaji Mkuu amesema ujenzi huo unahusisha karakana (Depot) moja, vituo vikuu (terminals) mbili na vituo mlisho (feeder stations) nne.

Amesema awamu ya pili inatekelezwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), African Growing Together (AGTF) na mchango wa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya fidia.

Post a Comment

Previous Post Next Post