Na John Nditi, Morogoro
SERIKALI
imebaini uwepo wa mkakati wa kukwamisha kuanza kwa ujenzi wa viwanda
vingi vya kuchakata miwa ya wakulima ili nchi isijitosheleze kwa
uzalishaji wa sukari nchini .
Hivyo imewaonya watu wenye nia
hiyo pamoja na viwanda vya sukari vinavyoshiriki kukwamisha kuanzishwa
kwa viwanda vingi vya kuchakata miwa kuacha mara moja njama hizo
vinginevyo wanakuwa wanakalia kaa la moto.
Waziri wa Kilimo,
Profesa Adolf Mkenda, alitoa onyo hilo alipotembelea Kiwanda cha
Mkulazi II na kuzungumza na wakulima wa miwa kutoka vijiji vya
Msowero, Malangali, Mvumi,Wami Dakwa na Mbigiri vilivyopo katika
wilaya ya Kilosa.
Alisema kuwa kuna taarifa za uhakika kuwa
baadhi ya watu wasioitakia mema nchi wanakwamisha jitihada za kuanzishwa
kwa kiwanda cha kuzalisha sukari cha Mkulazi II hatua ambayo
inayoendelea kuwaumiza wakulima wa miwa kwa mazao yao kutupwa kwa kukosa
wanunuzi wa uhakika
“Nawahakikishia ninazo taarifa kwamba sasa
kiwanda kitakamilika na kuanza kazi haraka, kwa hiyo wakulima msiwe na
wasiwasi na soko la miwa” Profesa Mkenda aliwahakikishia wakulima wa
miwa bonde la Mbigiri wilayani Kilosa.
Waziri alisema kuwa,
anayezuia kiwanda hiki cha Mkulazi II kisianze kazi serikali itachukua
hatua kali na Serikali itapambana na changamoto zote zilizopo
kuhakikisha kuwa kiwanda kinafanya kazi.
“ Naomba niwashukuru
wakulima kwa uvumilivu mpaka hapo tulipofika na changamoto nyingi,lakini
nawahakikishia ninazo taarifa sasa kiwanda hapa kitakamilika na
kitaanza kufanya kazi na serikali haitawaangusha “alisema Profesa
Mkenda.
Waziri Mkenda , alisema ; “ sisi wote tutasimama nao
zile changamoto ambazo zingine hawajazisema tutapambana nazo,anayezuia
kiwanda hiki kisifanye kazi ‘tutampasua’ tunajua nini kinaendelea
tunapambana na mambo mengi sana hiki kiwanda kitaanza kazi” alisema
Profesa Mkenda.
Waziri Mkenda , alisema kwa muda wa miaka
mitatu sasa tangu mwaka 2018 wakulima wa miwa wa Bonde la Mbigiri wilaya
ya Kilosa wamekuwa wakihangaika kuuza miwa yao kutokana na kiwanda cha
Mkulazi kushindwa kukamilika huku wakulima wakiendelea kudaiwa mikopo ya
fedha walizokopeshwa na Benki ya Azania
“ Anayesimama kuzuia
hiki kiwanda kisifanye kazi sSerikali itamshangaza kwa kuwa inapambana
na mambo mengi makubwa na imekuwa ikishinda”alisema Profesa Mkenda.
Waziri huyo alivitaka viwanda vya sukari vya Kilombero na Mtibwa
vianze kujitathimini kutokana na kushindwa kununua miwa yote ya wakulima
wa nje kutokana uwezo mdogo wa uchakataji wa miwa huku serikali ikiwapa
vibali vya kuagiza sukari kutoka nje ili kuziba pengo linalojitokeza.
“
Tuna maslahi kama serikali kuhakikisha kwamba tunajitosheleza kwa
sukari , maslahi yetu katika soko la sukari yanarandana na maslahi
mapana ya mkulima wa miwa kupata soko na serikali kujitegemea kwenye
sukari” alisititiza Profesa Mkenda.
Naye Mbunge wa Jimbo la
Mikumi ,Dennis Londo,akizungumza kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la
Kilosa,Profesa Palamagamba Kabudi ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,alisema licha ya wakulima wake
kuhamasika kulima miwa lakini hawana uhakika wa soko la miwa kwa kipindi
cha miaka mitatu.
Mbunge huyo ,alisema kukosekana kwa uhakika
huo kunatokana na kucheleweshwaji wa ukamilishwaji wa kiwanda cha
Sukari Mkulazi II na matokeo yake miwa yao kwenda kuuzwa kiwanda cha
Mtibwa kwa bei ya chini ya Sh : 60,000 hadi Sh : 65,000 kwa tani moja
ukilinganishwa na gharama za uzalishaji.
Mkulima wa miwa wa
Mbigiri Salome Mbilinyi ,alisema walihamasishwa kulima miwa katika
mashamba yao walikuwa wakilima mahindi lakini miwa hiyo imeshindwa
kufunwa miaka mitatu bila kuuzwa.
Mkulima mwingine Saidi
Mazunde wa Mbigiri alisema licha ya jitihada uongozi wa Mkulazi
kuwatafutia soko katika kiwanda cha Mtibwa baada ya kuuza miwa hiyo
wamekuwa wakikatwa benki ya Azania riba kubwa ya asilimia 50 badala ya
asilimia 25 ya makubaliano na nyingine ya asilimia sita (6) ya
adhabu ya kuchelewesha mkopo.
Mazunde , alisema kuwa tatizo la
kudaiwa kukatwa riba ya asilimia sita zaidi limetokana na mkataba kati
ya Kampuni ya Mkulazi , AMCOS na wakulima kuwa kitakapoanza kiwanda
wakulima wote watauza miwa yao huko , lakini sasa ni miaka mitatu
kiwanda hakijaanza na mkulima anaonekana kupewa adhabu.
“ Hii
asilimia 6 ya riba ya adhabu tunaomba ibebwe na Mkulazi kwa kuwa ndio
waliotushawishi tulime kwa kuwa wataanzisha kiwanda hapa Mbigiri”
alisema Mazunde.
Hata hivyo ,alisema kutokana kukosekana kwa
soko hivi sasa baadhi ya wakulima wa miwa wameanza kung’oa miwa na
kupanda mazao mengine ya kujikimu na kumuomba Waziri huyo kusimamia
uanzishwaji wa kiwanda hicho haraka.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ,Kilimo,Mifugo na Maji,Dk Christine
Ishengoma, aliwasihi wakulima wasikate tamaa kuacha kulima miwa na
wasing’oe miwa yao au kuanzisha kilimo cha mazao mengine kutokana na
kiwanda kuchelewa kuanza.
Dk Ishengoma aliwataka wawe
wavumilivu kwa kuwa Serikali ya awamu ya tano imepokea kilio chao kwa
Waziri wa Kilimo kuja kuwasilikiza . “Wakulima wangu msife moyo
mkachukua hatua za kuchimbua miwa,Tunataka kilimo kimkomboe mkulima
hivyo kwero zenu zitapatiwa ufumbuzi haraka.” Dk Ishengoma.
Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, akizungumza na wakulima wa miwa kutoka vijiji vya Msowero, Malangali, Mvumi,Wami Dakwa na Mbigiri vilivyopo katika wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro alipotembelea Kiwanda cha Mkulazi II kilichopo wilayani humo.
Baadhi ya viongozi wa Serikali na Taasisi za Umma pamoja na wadau wa tasnia ya Sukari wakimsililiza Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, ( hayupo pichani) wakati akizungumza na wakulima wa miwa kutoka vijiji vya Msowero, Malangali, Mvumi,Wami Dakwa na Mbigiri vilivyopo katika wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro alipotembelea Kiwanda cha Mkulazi II kilichopo wilayani humo.
Mmmoja wa wakulima wa miwa wa bonde la Mbigiri wilayani Kilosa , mkoa wa Morogoro akitoa kero zake na za wakulima wenzake kuhusiana changamoto mbalimbali katika kilimo cha miwa .( Picha na John Nditi).