Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetia saini mkataba wa Ujenzi wa Mradi wa Maji
kutoka Ziwa Victoria kwenda katika Miji ya Tinde katika halmashauri ya wilaya
ya Shinyanga na Shelui wilaya ya Iramba mkoani Singida utakaotekelezwa kwa
kipindi cha miezi 12 ukigharimu Jumla ya shilingi Bilioni 24.4.
Hafla ya Utiaji
Saini Mkataba wa Ujenzi wa Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika
Miji ya Tinde na Shelui imefanyika leo Alhamisi Februari 25,2021 katika Mji wa
Tinde na kushuhudiwa na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso na wananchi na viongozi mbalimbali
wa mkoa wa Shinyanga na Singida.
Mkataba huo
umesainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga na Naibu
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Megha Engineering
and Infrastructures Ltd katika Miji ya Tinde na Shelui,bwana Murali Mohan.
Akitoa
taarifa kuhusu mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga
amesema mradi huo unaotarajiwa kutatua kero ya maji katika Miji ya Tinde
na Shelui unatekelezwa kwa fedha za mkopo wa masharti nafuu kutoka
serikali ya
India kupitia Exim Bank India.
“Kazi
zilizopangwa kutekelezwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha kusukuma maji katika
mji wa Tyeme kata ya Shelui,kulaza bomba kuu (Transmission main) lenye ukubwa
kati ya milimita 400 na 300 kutoka bomba kuu kijiji cha Chembeli hadi Tinde
lenye urefu wa kilomita 20.93 na bomba la ukubwa wa milimita 50 kwenye tanki la
Didia lenye urefu wa kilomita 1.5”,amesema Mhandisi Sanga.
“Shughuli
nyingine ni kulaza bomba kuu lenye ukubwa wa kati ya milimita 350 na 200 kutoka
bomba kuu linalokwenda Igunga katika kijiji cha Ipumbulya hadi Mgeta, Shelui
lenye urefu wa kilomita 70.5,kujenga matanki ya kuhifadhia maji,ukaratabati wa
matanki na kujenga vituo vya kuchotea maji”,amesema.
Kwa upande
wake, Waziri wa Maji , Jumaa Aweso amesema ujenzi wa mradi huo ni sehemu ya
utekelezaji wa Agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe
alilotoa Januari 29,2021 alipopita Tinde na Shelui ambapo alitaka wananchi wa
maeneo hayo wapewe huduma ya Maji kutoka Ziwa Victoria.
“Hili ni
Jambo kubwa sana na tunamshukuru Mhe. Rais Magufuli. Nimuombe Mkandarasi
anayejenga mradi huu kuhakikisha anafanya kazi kwa kuzingatia mkataba wa mradi
na kuhakikisha anamaliza ndani ya miezi 12. Niwaambie tu kuwa hatutaongeza muda”,amesema
Aweso.
“Mkandarasi
hakikisha unamaliza ujenzi kwa wakati kwa kuzingatia mkataba na fedha zitumike
kama ilivyopangwa na ikiwezekana chenji ibaki”,ameongeza.
Aidha
amesema hatamvumilia mtu yeyote atakayethubutu kuhujumu mradi huo akiwataka
wananchi kushirikiana na mkandarasi
“Huu ni mradi wangu wa kwanza kusainiwa
nikiwepo, Msichezee huu mradi, ukishiba chezea kitambi chako au kidevu chako. Mimi
ni Waziri Kijana atakayezingua tutazinguana. Ninachotaka wananchi wapate maji
safi na salama kwa gharama nafuu”, amesisitiza Aweso.
Kwa upande
wake, Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko alimuomba Waziri wa Maji
kuingiza kwenye bajeti za mradi kata za Nsalala, Usule na Bukene kwani
zimerukwa katika mradi huo ambapo Waziri
Aweso alisema kata ya Nsalala pia itanufaika katika mradi huo wa maji kutoka
Ziwa Victoria kwenda Tinde na Kiomboi.
Mkuu huyo wa
wilaya alitumia fursa hiyo kuzipongeza mamlaka za maji SHUWASA na KASHWASA kwa
kazi nzuri wanazofanya katika huduma za maji kwenye wilaya ya Shinyanga.
Naye Mkuu wa
Wilaya ya Iramba, Mhe. Emmanuel Ruhahula amesema mradi huo wa maji utasaidia
kwa kiasi kikubwa kupunguza adha ya maji katika mji wa Shelui.
Mkuu wa Mkoa
wa Shinyanga, Mhe. Zainab Telack amewataka wananchi kulinda miundombinu ya
mradi huo wa maji na kuhakikisha wanashiriki katika ujenzi wa mradi ili kuondoa
changamoto ya maji kwa wananchi.
Mbunge wa
Jimbo la Solwa Mhe. Ahmed Salum ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Magufuli
kutatua changamoto ya maji katika mji wa Tinde akiomba pia kata zilizosahaulika
ziingizwe kwenye mradi na kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi wa maji katika
kata ya Mwakitolyo.
Nao wananchi
wa Tinde akiwemo aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Shinyanga Azza Hilal
wamesema kukamilika kwa mradi wa maji katika mji wa Tinde kutachochea maendeleo
ya Tinde kwani yalisimama kutokana na changamoto ya maji.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI