Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi akikagua ujenzi wa tenki la maji la Buswelu katika Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela lenye ujazo wa lita milioni tatu.
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi akiteremka kutoka kwenye tenki baada ya kukagua ujenzi wa tenki hilo linalojengwa juu ya mlima unaoitwa wa DC Ilemela, tenki hilo likikamilika litahudumia wananchi wa maeneo ya Buswelu, Lukobe, Kigala, Nsumba Kahama, Bujigwa, Nyadadoke na Ilalila.
Baadhi ya viongozi aliombatana nao Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi wakiteremka kutoka kukagua tenki la maji lenye ujazo wa lita milioni 3 linalojengwa juu yam lima wa DC Ilemela.
Tenki la maji linalojengwa juu ya mlima wa DC likiwa limefikia asilimia 15 katika utekelezaji wake.
………………………………………………………………………………………
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya maji hapa nchini kukamilisha kwa wakati ili wananchi wapate huduma ya majisafi na salama.
Waziri Mahundi amesema hayo kwa nyakati totauti wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maji katika Wilaya ya Nyamagana na Ilemela ambako alikagua miradi miwili inayotekelezwa kwa ajili ya kuongeza kasi ya upatikanaji wa maji katika maeneo hayo.
Amesema wakandarasi ambao watachelewesha miradi serikali itafuatilia kujua ukomo wao wa mikataba na hakutakuwa na muda wa nyongeza labda tu kuwe na sababu za msingi zilizosababisha mradi kuchelewa.
“Hatutawaongezea muda wakandarasi wote watakaoshindwa kukamilisha miradi kwa wakati kama mikataba yao inavyosema na badala yake kazi hizo zitafanywa kwa kutumia wakandarasi wa ndani (force Account) ili miradi ikamilike na wananchi wapate huduma ya majisafi na salama na yenye kutosheleza”, Mhe. Mhandisi Mahundi amesisitiza.
Aidha, Naibu Waziri amemuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) Mhandisi Leonard Msenyele kuhakikisha kwamba miradi ya maji inapokamilika wananchi wanaunganishiwa maji majumbani.
“Suala la kupeleka maji majumbani na lenyewe mlipe kipaumbele mara miradi ya maji inapokamilika, toeni kipaumbele kwa wale wanaohitaji kuunganishiwa majumbani”, amesema Mhe. Mhandisi Mahundi.
Mkataba wa utekelezaji wa mradi wa kulaza bomba kuu la maji kutoka chanzo kipya cha maji eneo la Butimba hadi Igoma ulisainiwa kati ya MWAUWASA na Kampuni ya Ki-China CCECC ambao ulianza kutekelezwa tarehe 01 Novemba, 2019 na kufikia Januari, 2021 mradi umefikia asilimia 50 na unategemewa kukamilika mwezi Oktoba, 2021. Hadi kufikia Januari, 2021 Mkandarasi ameshalipwa Euro milioni 2.6 sawa na asilimia 40.
Mradi huu ukikamilika utaboresha huduma ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wapatao 105,649 waishio katika maeneo ya Nyegezi, Buhongwa, Kanyerere, Sahwa, Lwanhima, Kanindo, Fumagila, Igoma na Buswelu.
Aidha, mradi wa ujenzi wa tenki la majisafi la Buswelu lenye ujazo wa lita milioni 3 umeanzwa kutekelezwa tarehe 15 Septemba, 2020 na unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Juni, 2021 ambapo kwa sasa umefikia asilimia 15 na unatekelezwa na Mkandarasi China Civil Engineering Construction kwa gharama ya shilingi bilioni 5.1. Tenki hili likikamilika litahudumia wananchi wa maeneo ya Buswelu, Lukobe, Kigala, Nsumba Kahama, Bujigwa, Nyamadoke na Ilalila.