MRADI WA NYUMBA ZA MAKAZI MAGOMENI KOTA RASMI KUKAMILIKA MWEZI APRILI MWAKA HUU

  Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya akiongozana na watumishi wa Wakala wa Majengo TBA akikagua mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya Magomeni Kota leo Jijini Dar es Salaam.Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya  (katikati) akimsikiliza Meneja anayesimamia mradi wa ujenzi wa makazi Magomeni Kota Bw.Bernard Mayemba mara baada ya kutembelea mradi huo leo Jijini Dar es Salaam. 

Meneja anayesimamia mradi wa Magomeni Kota Bw.Bernard Mayemba akimuelezea Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya namna mradi huo ulipofikia mara baada ya kutembelea mradi huo leo Jijini Dar es Salaam.

************************************ 

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MRADI wa nyumba za makazi wa Magomeni Kota umekamilika kwa asilimia 91 huku ukitarajiwa kupokea kaya zipatazo 644 kama ilivyoelekezwa na Rais Dkt.John Joseph Magufuli mnamo Oktoba, 2016.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea mradi huo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema, mradi huo unaenda vyema na katika ubora walioutarajia na maagizo yote yaliyotolewa na viongozi mbalimbali wa Serikali waliotembelea mradi huo yametekelezwa.

Kasekenya amesema, mapema Aprili wakazi waliokuwa wakiishi katika eneo hilo watarudi na kuendelea kuishi katika kota hizo zilizojengwa kisasa.

“Hali imebadilika, TBA wameongeza ubunifu kwa kuongeza makazi ya kaya 14 zaidi katika majengo haya, hata ningekua mimi ningerudi hapa…ni nyumba za kisasa na huduma zote muhimu zimesogezwa kuna sehemu za kucheza watoto, maduka pamoja na sehemu maalumu kwa ajili ya ulinzi. Hakika tunashukuru Rais Magufuli kwa maono, maamuzi na utekelezaji bora wa ilani ya Chama cha Mapinduzi.” Amesema Kasekenya.

Aidha ameipongeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) kwa kuongeza ubunifu katika mradi huo uliosimamiwa na watanzania kwa asilimia 100 na kuwataka kuendelea kutekeleza miradi ya namna hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.

“TBA mnafanya kazi nzuri endeleeni kutekeleza miradi ya namna hii zaidi, mkawekeze katika maeneo mengi zaidi kama mlivyofanya hapa Magomeni Kota tumeona familia moja itakuwa na vyumba viwili vya kulala, sebule, choo, bafu, jiko na sehemu maalumu ya kufulia.” Amesema.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Mbunifu Majengo Daud Kondoro amesema, kukamilika kwa mradi huo kwa asilimia 91 ni matokeo ya kufanya kazi usiku na mchana katika kuhakikisha azma na ahadi ya Rais Magufuli ya kutoa makazi bora kwa wakazi wa eneo hilo unakamilika.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja anayesimamia mradi huo Bernard Mayemba amesema, Wakala ya Majengo Tanzania (TBA,) imejipanga katika uwezeshaji na utekelezaji wa miradi mingi zaidi nchini.

Pia amesema, mifumo awali ya umeme na maji umekamilika na hiyo ni pamoja na sehemu maalumu ya walinzi ambao watalinda makazi na wakazi wa eneo hilo kwa saa 24.

“Tupo katika hatua za umaliziaji katika nakshi za mandhari ya Majengo na sakafu..pesa na vifaa vipo na ifikapo Aprili wakazi wa eneo hilo wataanza kuishi katika makazi hayo.” Amesema.

Mayemba amesema kuwa mradi huo umekuwa na manufaa kwa wakazi wa maeneo hayo ambapo kwa siku takribani vijana 700 hadi 800 wamekuwa wakipata ajira katika eneo hilo usiku na mchana.

Mradi wa Ujenzi wa nyumba za makazi Magomeni Kota unasimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) kwa Fedha za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa gharama ya shilingi 50,586,997,000.00.

Post a Comment

Previous Post Next Post