Na John Nditi, Morogoro
WAZIRI wa Kilimo,Profesa Adolf Mkenda,amezishauri Taasisi za Fedha kutoa mikopo kwa wanaotaka kuwekeza kwaajili ya kuanzisha viwanda vya sukari ili kuleta ushindani na viwanda vya sukari vilivyopo kwa lengo la kujitosheleza kwa sukari hapa nchini.
Profesa Mkenda alisema hayo wakati akielezea mwenendo wa uzalishaji wa sukari na kilimo cha miwa kwa wakulima wa nje wa miwa na uongozi wa kiwanda cha sukari cha Mtibwa kilichopo wilayani Mvomero,mkoani Morogoro.
Waziri, alisema kuwa kutokana na viwanda vya sukari vilivyopo hivi sasa kutokuwa na uwezo wa kuchakata miwa yote ya wakulima ,Serikali imeamua kushawishi wawekezaji wakiwemo wajasiliamali wanaohitaji kuwekeza katika viwanda vya sukari kujitokeza na serikali itawashika mkono kwa kuhakikisha wanapata mikopo.
“Tunahitaji wawekezaji wengi kwa ajili ya kuanzisha viwanda vya sukari na sisi kama serikali tutahakikisha Taasisi za fedha ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo inatoa mikopo kwa wenye nia ya kujenga viwanda hivyo” alisema Waziri Mkenda.
Waziri Mkenda ,alisema; “ lengo ni kuleta ushindani na hilo ndio litakuwa jawabu la kutatua changamoto ya wakulima miwa yao kutopata soko “ alisema Waziri huyo.
Hivyo alitoa wito kwa wajasilimali wanaohitaji kuanzisha viwanda vidogo vya kuchakata sukari waende kuzungumza na mabenki ili yawasaidie kupata mikopo ili wawekeza na kumaliza tatizo la upungufu wa sukari na kuwepo soko la uhakika la miwa.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Mvomero,Jonas Van Zeland,alisema wakulima wa miwa katika wilaya hiyo wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo miwa kununuliwa kwa bei ya chini ambapo tani moja ununuliwa kwa shilingi 65,000 tofauti na wakulima wa wilaya ya Kilombero ambao tani moja inanunuliwa na kiwanda shilingi 110,000 wakati ni mkoa mmoja wenye viwanda vya sukari.
Mbunge huyo wa Mvomero, alisema ili kuleta ushindani ni vyema serikali ikaruhusu ujenzi wa viwanda vingine vidogo kwenye eneo la viwanda vikubwa ili wakulima wachaguwe eneo la kupeleka miwa yao hatua ambayo italeta ushindani na suruhisho la matatizo ya wakulima.
Mmoja wa wakulima wa miwa Seif Hassani kutoka kijiji cha mapambano wilayani humo,alisema licha ya kuzalisha miwa lakini mifugo imekuwa ikiwapa hasara kutokana wafugaji kuingiza mifugo nyakati za usiku katika mashamba ya wakulima na hivyo kuleta uhalibifu unaosababisha wapate hasara kwakuwa kilimo wanachofanya kimekuwa kikitumia mikopo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo,Mifugo na Maji,Dk Christine Ishengoma,alisema wameshapokea malalamiko kutoka kwa wakulima wa wilaya ya Mvomero ikiwemo bei ya chini ya miwa inayotolewa na mwekezaji wa kiwanda cha Mtibwa wakati mkulima kama huyo katika wilaya ya Kilombero analipwa bei ya juu na suala tayari wameshalifikisha serikalini kwaajili ya kupatiwa ufumbuzi.
Alisema kero nyingine ambayo kamati yake ni uwepo wa mifugo unaosababisha kuharibu mashamba ya miwa ingawa kwa sasa imeripotiwa kupungua lakini bado ipo na kuleta changamoto kwa wakulima .
“ Waziri wa kilimo kama changamoto hizo za wakulima wa miwa katika wilaya ya Mvomero hazitapatiwa ufumbuzi itawarudisha nyuma na hivyo kuacha kuendelea na kilimo cha miwa na kuamia kwenye mazao mengine ikiwemo mpunga na hivyo kuifanya adhma ya serikali ya kujitosheleza kwa sukari kutofanikiwa” alisema Dk Ishengema ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Morogoro.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo, (TADB), Japhet Justine ,alisema wapo tayari kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanaotaka kuanzisha viwanda vya kuchakata miwa kulingana na andiko la mradi wa aina ya kiwanda kinachotakiwa kujengwa.
Alisema kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za fedha katika kuwawezesha wenye nia ya kuanzisha viwanda wajitokeze kutumia fursa zilizopo kwakuwa nchi inahitaji kumaliza tatizo la upungufu wa sukari.
Waziri wa Kilimo Profesa, Adolf Mkenda ( kushoto aliyeshika mlango wa kufungulia maji ) akikagua banio la skimu ya umwagiliaji ya kijiji cha Msolwa Ujamaa katika wilaya ya Kilombero , mkoani Morogoro iliyojngwa chini ya Mradi wa Kuongeza Tija na Uzalishaji Mpunga (ERPP) ambapo ameagiza wakulima kutunza miundombinu hiyo( kulia aliyeshika mlango wa maji ) ni Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Gerald Kusaya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo, (TADB), Japhet Justine akizungumza na waandishi wa habari wakiwa wilayani Mvomero juu ya Benki hiyo ilivyoweka mpango mkakati na kipaumbele cha utaoji mikopo kwa wawekezaji na wajasiliamali kwenye sekta ya Kilimo hususani tasnia ya sukari. ( Picha zote na John Nditi).
Waziri wa Kilimo Profesa, Adolf Mkenda akieleza jambo wakati akizungumza na viongozi wa Serikali ya wilaya ya Mvomero , Mkoani Morogoro ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya hiyo, Albinus Mgonya ( wa kwanza kushoto) alipokuwa kwenye ziara ya kukagua hali ya uzalishaji sukari na kuongea na wakulima wa miwa wilayani humo na (wapili kulia ni ) Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Jonas Van Zeeland na ( wa kwanza kulia) ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Yusuf Makunja.
Waziri wa Kilimo Profesa, Adolf Mkenda akizungumza jambo na wakulima wa miwa wilaya ya Mvomero kwenye ukumbi wa Mtibwa alipokuwa kwenye ziara ya kukagua hali ya uzalishaji sukari na kuongea nao (wa kwanza kulia ) ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na Maji , Dk Chiristine Ishengoma na (wapili kulia) Katibu mkuu wa wizara hiyo , Gerald Kusaya na ( kushoto kwa waziri) ni Mkuu wa wilaya ya Mvomero ,Albinus Mgonya .
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo, (TADB), Japhet Justine ( wa kwanza kulia mstari wa mbele ) akimsililiza Waziri wa Kilimo Profesa, Adolf Mkenda ( hayu pichani ) alipokuwa akizungumza na viongozi wa Serikali ya wilaya ya Mvomero , Mkoani Morogoro na uongozi wa kiwanda cha Sukari Mtibwa wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya uzalishaji sukari na kuongea na wakulima wa miwa wilayani humo.
Mmoja wa wakulima wa zao la miwa katika tarafa ya Turiani , wilayani Mvomero akitia kero zake kuhusu changamoto ya kilimo cha miwa mbele ya Waziri wa Kilimo ,Profesa Adolf Mkenda ( hayupo pichani) wakati wa ziaraya kukagua hali ya uzalishaji sukari na kuongea na wakulima wa miwa wilayani humo.