KASEKENYA AAGIZA TANROADS KURUDISHA MAWASILIANO DARAJA LA MTO ITUMBA

 

Muonekano wa daraja linalounganisha Kijiji cha Ilulu na Chagu, Wilayani Ileje, Mkoani Songwe lililovunjika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani humo. Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imeahidi kushughulikia daraja hilo ili kurejesha mawasiliano.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Godfrey Kasekenya (aliyevaa miwani), akiangalia uharibifu uliotokea katika daraja linalounganisha Kijiji cha Ilulu na Chagu, Wilayani Ileje, Mkoani Songwe. Daraja hilo limevunjika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani humo.

Muonekano wa daraja linalounganisha Nchi ya Tanzania na Malawi, Wilayani Ileje, Mkoani Songwe likiwa limejaa maji kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani humo.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akizungumza na mkazi wa nchini Malawi, aliyekwama mpakani mwa Tanzania na Malawi kutokana changamoto ya maji kupita juu ya daraja, na kusababisha kukoseakana kwa huduma za usafiri miongoni mwa nchi hizo, kupitia Wilayani Ileje, Mkoani Songwe.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya akisisitiza jambo kwa wakazi wa kata ya Mbebe, wilayani Ileje, Mkoani Songwe, alipozungumza nao hivi karibuni.

Baadhi ya wananchi wa kata ya Mbebe, wilayani Ileje, Mkoani Songwe, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (hayupo pichani), alipozungumza nao kuhusu maendeleo ya miundombinu katika mkoa huo, hivi karibuni.

PICHA NA WUU

*********************************

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi, Godfrey Kasekenya, ameuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoani Songwe, kuhakikisha unarudisha haraka mawasiliano yaliyokatika kutokana na kuvunjika kwa daraja la Mto Itumba kulikosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Mbebe, wilayani Ileje, mkoani humo, Kasekenya amesema kuwa jana alifika eneo la tukio na kukuta daraja hilo linalounganisha kijiji cha Chagu na Ilulu  limekatika na wananchi kushindwa kuvuka na hivyo kuamua kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuagiza TANROADS kutafuta njia ya haraka itakayorudisha mawasiliano katika vijiji hivyo.

“Jana jioni nilitembelea pale daraja la mto Itumba na Ieo hii  ni siku ya pili bado wananchi wanashindwa kuvuka kutokana na kukatika kwa daraja hili, kushindwa kwao kuvuka kunawakosesha huduma za kijamii, hivyo nichukue fursa hii kuwasisitiza TANROADS kuhakisha wanarudisha mawasiliano katika eneo hili haraka iwezekanavyo”, amesema Kasekenya.

Aidha, ameutaka pia Wakala wa Barabara za mijini na vijijini (TARURA) mkoani Songwe  hususan katika wilaya ya Ileje, kusimamia vizuri miradi yake ikiwemo madaraja na barabara  na  kuhakikisha inapitika katika majira yote kwani wananchi wamekuwa wakilalamika changamoto mbalimbali ikiwemo njia nyingi kutopitika kutokana na uharibifu wa miundombinu.

Katika hatua nyingine, Kasekenya amewataka wataalamu wa Idara mbalimbali wa Halmashauri kuweka utaratibu wa mara kwa mara wa kukutana na wananchi ili kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.

“Uwepo wa kero nyingi kutoka kwa wananchi kunasababishwa na kutokuwa na ratiba za mara kwa mara za kufanya mikutano na wananchi,niwaombe viongozi wa Halamashauri tokeni na msikilizeni kero ili muweke mikakati ya kuzitafutia majawabu mapema, msisubiri mpaka viongozi wa kitaifa waje”, amesema Kasekenya.

Kwa upande wake, mwanakiji wa Kata ya Mbebe,  akizungumza kwa niaba ya wanakijiji wengine, Bw. Ally Kalinga, amemeueleza Naibu Waziri huyo kuwa, miundombinu mingi hususan ya barabara na madaraja imekuwa ikiharibika sana hususan kipindi cha mvua na hivyo kusababisha kukosekana kwa huduma muhimu za kijamii kama vile elimu na afya.

Amemuomba Naibu Waziri kuboresha miundombinu hiyo ikiwemo kuijenga upya kwani  sehemu nyingine miundombinu hiyo ni chakavu na imechoka pia mingine haina ubora kulingana na uhitaji.

Naibu Waziri Kasekenya, amefanya ziara katika wilaya ya Ileje, mkoani Songwe, ambapo pamoja na mambo mengine, amefika wilayani hapo kwa ajili ya kuzungumza na wananchi wa jimbo lake ili kusilikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi. 

Post a Comment

Previous Post Next Post