NAIBU WAZIRI KIPANGA AAGIZA KUWEKWA NDANI MKANDARASI ANAEJENGA CHUO CHA UALIMU MPWAPWA

 

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Juma Kipanga (kushoto) akipewa ufafanuzi kwenye michoro ya majengo kutoka kwa wahusika wa kampuni ya CF Builders  ambao ndio wanaotekeleza ujenzi wa majengo matano mapya katika chuo cha ualimu Mpwapwa.
Mkandarasi Fredy Chacha na wasimamizi wawili, Thobias Ntobi na Laurent Vicent wote wa kampuni ya CF Builders wakiwa ndani ya gari la Polisi wakipelekwa kituo cha polisi.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga (kushoto) akizungumza na Mafundi na Vibarua wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa majengo mapya matano katika Chuo cha Ualimu Mpwapwa.
 
Muonekano wa jengo moja la nyumba za walimu lenye uwezo wa kuchukua familia tatu linalojengwa katika chuo cha ualimu Mpwapwa.

……………………………………………….

NAIBU  Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga ameagiza kuwekwa ndani kwa masaa 17 mkandarasi na wasimamizi wa mradi wa ujenzi wa majengo matano mapya katika Chuo cha Ualimu Mpwapwa baada ya kushindwa kutekeleza maagizo yaliyotolewa awali.

Mhe. Kipanga amewaweka ndani mmoja wa wakurugenzi wa kampuni CF Builders ya jijini Mwanza, Fredy Chacha na wasimamizi wa mradi huo Mhandisi Laurent Vicent na Thobias Ntobi wote wa kampuni hiyo iliyopewa kazi ya kujenga Mradi huo baada ya kushindwa kutoa sababu zilizopelekea wao kutotekeleza maagizo aliyoyatoa Desemba 19, 2020 na kusababisha mradi huo kusuasua.

Naibu Waziri Kipanga amesema mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 2.8 ulipaswa kukamilika tangu mwaka jana lakini mpaka sasa umetekelezwa kwa asilimia 16 tu huku kampuni hiyo ikiwa imeshalipwa zaidi ya asilimia 20%.

Amesema Desemba 19 alitoa maagizo mbalimbali kwa kampuni hiyo ikiwemo kuhakikisha vifaa vyote vya ujenzi vinakuwa eneo la ujenzi pamoja na kuongeza watumishi wa kutosha jambo ambalo wamelikaidi.

“Kwa kuwa nilikuja hapa tarehe 19 mwezi uliopita  na kuwapa maagizo ambayo naona hamjataka kuyatekeleza, sasa mtakwenda kulala ndani mpaka kesho saa nne kamili na mnapotoka ndani mtakuja moja kwa moja site kwa ajili ya kuandaa mpango wa manunuzi wa vifaa vyote vinavyohitajika na nataka niupate kimaandishi ifikapo kesho saa 10 jioni,” amesisitiza Naibu Waziri.

Aidha, Mhe Kipanga amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha anaongeza vibarua na mafundi wanaotoka katika maeneo ya Mpwapwa na kuhakikisha anawalipa vizuri ili kuwezesha kazi hiyo kwenda kwa kasi.

Kiongozi huyo amesema mradi huo ambao ulianza kutekelezwa tangu 2019 umekuwa ukisuasua bila sababu yeyote huku fedha za kukamilisha mradi huo zipo na  amewataka wataalamu wote wanaohusika na usimamizi wa mradi huo kuanza kufuatilia kwa karibu ili kuhakkikisha mpaka kufikia mwezi wa sita mwaka huu uwe umekamilika.

Awali Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa Mhe. George Malima alimweleza Naibu Waziri kuwa walikuwa na wasiwasi juu mkandarasi huyo katika kutekeleza mradi huo kwani muda mwingi amekuwa haonekani eneo la tukio. Amesema mara kadhaa amekuwa akifuatilia ujenzi huo lakini hakuna kilichokuwa kikiendelea.

Mhe. Malima amesisitiza umuhimu wa mradi huo kukamilika mapema kwa kuwa utaongeza idadi ya wanachuo ambao uwepo wao utasaidia kukuza uchumi wa eneo hilo na ameahidi kusimamia mradi huo mpaka utakapokamilika.

Naye Mkuu wa Chuo cha Ualimu Mpwapwa, Gerald Richard amemweleza Naibu Waziri kuwa mradi huo ambao ualianza mwaka wa fedha 2018/19 unahusisha ujenzi wa majengo mapya matano ambayo ni pamoja na jengo la ghorofa moja kwa ajili ya idara ya Teknolojia ya Habari, na Mawasiliano (TEHAMA), Bweni la ghorofa moja kwa ajili ya wanachuo wa kike, ukumbi wa chakula na nyumba mbili za watumishi ambapo nyumba moja ina uwezo wa kuchukua familia tatu.

Post a Comment

Previous Post Next Post