Bohari ya Dawa (MSD) imeshinda tuzo ya Huduma kwa Wateja katika sekta ya Dawa na Vifaa Tiba.
Tuzo hiyo ilitolewa tarehe 13 Februari 2026 katika ukumbi wa King Jada Hotel na taasisi ya kimataifa inayojishughulisha na utoaji wa mafunzo, vyeti na viwango vya taaluma ya huduma kwa wateja na vituo vya kupokea simu ijulikanayo kama Chartered Institute of Customer Management (CICM) Tanzania.
Tuzo hii inaonesha namna MSD ilivyoboresha huduma zake kwa wateja, hususan katika upatikanaji wa bidhaa za afya kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini.
Hadi sasa MSD inahudumia vituo vya kutolea huduma za afya 8,893 nchi nzima, huku vituo vyote vikipelekewa bidhaa hizo hadi mlangoni mara sita kwa mwaka.
Mkurugenzi wa Ugavi na Uendeshaji, Hassan Ali, ameeleza kuwa tangu kufanyika kwa maboresho ndani ya Bohari ya Dawa, bidhaa za aina mbalimbali zimekuwa zikisambazwa kuendana na kasi ya uhitaji wa huduma hizo. Bidhaa hizo ni pamoja na mashine za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo, mashine za usingizi, pamoja na zile za kuwezesha huduma za afya ya kinywa na meno, ambapo huduma zote hutekelezwa kwa kuzingatia misingi ya huduma bora kwa wateja iliyowekwa.
Ameongeza kuwa MSD ina mifumo ya kisasa ya kuwasiliana na wateja kama vile Customer Portal, ujumbe mfupi wa simu (Bulk SMS), pamoja na Call Center, mifumo ambayo huwezesha mawasiliano ya haraka na utatuzi wa changamoto mbalimbali kwa wateja.

