MTANDAO WA BARABARA NCHINI WAIMARIKA

 

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Leonard Chamuriho, akifafanua jambo mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, jijini Dodoma.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, akifafanua jambo kwa Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Leonard Chamuriho, wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya Wizara yake kwa kamati hiyo, jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, akisoma taarifa ya utendaji kazi wa TANROADS mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, jijini Dodoma.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Wakurugenzi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, wakisikiliza taarifa ya Utendaji kazi wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) iliyosomwa na Mhandisi Patrick Barozi (aliyesimama), jijini Dodoma.

………………………………………………………………………………

Imeelezwa kuwa ubora wa mtandao wa barabara za Kitaifa umeimarika na kufikia wastani wa asilimia 87 na za Wilaya zimefika asilimia 56 kwa barabara zilizo kwenye hali nzuri na wastani kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015/16 hadi 2019/20.

Akizungumza katika kikao cha pili cha kamati ya Bunge ya Miundombinu Bungeni jijini Dodoma, ambapo Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Leonard Chamuriho amesema kuwa hali hiyo imetokana na mtiririko mzuri wa fedha kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara (RfB) kwenda kwa Wakala wa Barabara (TANROADS). 

Aidha, Chamuriho ameieleza Kamati hiyo kuwa Wizara imeendelea kuzisimamia Taasisi zake ili kuhakikisha kuwa fedha zinazotolewa zinatumika kikamilifu katika miradi iliyokusudiwa.

“Katika mwaka wa fedha 2020/21 Wizara imeidhinisha mpango wa manunuzi wa TANROADS (Procurement Plan), kwa ajili ya miradi 56 ambapo kati ya hiyo miradi 41 ni ya barabara, miradi 11 ya Viwanja vya Ndege, miradi mitatu ya ujenzi wa madaraja pamoja na mradi mmoja wa ujenzi wa Mizani”, alisema Mhandisi Chamuriho. 

Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Patric Mfugale, aliieleza kamati hiyo kuwa hadi kufikia Desemba, 2020, Wakala umepokea jumla ya Shilingi milioni 226,654.062 kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara ambayo ni sawa na asilimia 40 ya bajeti ya mwaka 2020/21.

Akifunga kikao hicho Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Mama Anne Kilango Malechela, ameitaka Wizara hiyo kusimamia kwa karibu suala la magari yanayozidisha uzito kwani yamekuwa yakichangia kwa kiwango kikubwa uharibifu wa barabara ambapo ujenzi wake umeigharimu serikali fedha nyingi.

“Hadi sasa eneo la mizani bado halijasimamiwa vizuri na hivyo juhudi ziongezwe ili kuhakikisha magari hayazidishi uzito, kwani fedha zinazo patikana kutokana na faini ya kuzidisha uzito wa magari barabarani hazitoshi ukilinganisha na uharibifu mkubwa wa barabara unaofanywa na magari hayo”, alisema Malechela

Wizara kupitia taasisi zake iliwasilisha Taarifa mbalilibali ikiwemo taarifa za utendaji kutoka Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB) pamoja na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB).

Post a Comment

Previous Post Next Post