MKANDARASI APEWA SIKU 60 KUKAMILISHA UJENZI WA TENKI LA MAJI LA BUIGIRI – CHAMWINO

 

Muonekano wa eneo kunakojengwa tenki la maji la Buigiri Wilayani Chamwino.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba akiangalia eneo la Hospitali ya Rufaa ya Uhuru litakalopitiwa na miundombinu ya maji kutoka tenki la maji lililoko eneo la Buigiri Wilayani Chamwino alipofanya ziara ya kikazi jijini Dodoma leo.

Muonekano wa Hospitali ya Rufaa ya Uhuru iliyopo jijini Dodoma itakayotumia maji kutoka tenki la maji lililoko eneo la Buigiri Wilayani Chamwino.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba (wa pili kutoka kushoto) akitoa maelekezo kwa mkandarasi SUMA-JKT kukamilisha ujenzi wa tenki la maji la Buigiri – Chamwino alipokagua ujenzi wa tenki hilo jijini Dodoma leo. Wengine ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira  Mjini Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph (wa kwanza kushoto) na baadhi ya watendaji wa DUWASA.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) alipofanya ukaguzi wa ujenzi wa tenki la maji lililoko eneo la Buigiri Wilayani Chamwino  jijini Dodoma leo.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba akiuliza maswali kuhusu ramani ya uchimbaji visima katika eneo la Ihumwa alipofanya ziara ya kikazi katika eneo hilo jijini Dodoma leo.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba (katikati) akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira  Mjini Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph (wa kwanza kushoto) alipokuwa akitoa  ufafanuzi kuhusu kazi ya flushing ya kisima katika eneo la Nzuguni Jijini Dodoma leo.

***********************************************************

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba ametoa siku 60 kwa mkandarasi SUMA-JKT kukamilisha ujenzi wa tenki la maji la Buigiri – Chamwino litakalogharimu kiasi cha shilingi milioni 998 linatarajiwa kuhudumia wakazi wa Chamwino na Hospitali ya Rufaa ya Uhuru jijini Dodoma.

Ametoa agizo hilo leo alipofanya ziara ya kikazi kukagua maendeleo ya ujenzi wa tenki hilo litakalokuwa na ujazo wa lita milioni mbili na laki tano lililoko eneo la Buigiri – Chamwino.

²Tumekubaliana na mkandarasi kuwa tenki hili likamilike ndani ya mwezi wa pili, kwa hiyo wana siku 60 tu kuhakikisha ujenzi umekamilika²

Naibu Katibu Mkuu, Kemikimba amesema kuwa ilitakiwa tenki hilo lijengwe tangu mwezi wa tisa mwaka 2020 lakini kutokana na mipango yao wenyewe imepelekea kuchelewa kwa ujenzi huo.

Aidha, ameitaka menejimenti ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Dodoma (DUWASA) kufanya ufuatiliaji wa ujenzi wa tenki hilo kila siku ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu, Kemikimba ametembelea eneo la Ihumwa panapochimbwa visima na amekiagiza kitengo cha uchimbaji kilicho chini ya RUWASA kuongeza kasi ya uchimbaji visima ili kukamilisha miradi kwa wakati lengo ikiwa ni kuongeza kiasi cha maji kwa Jiji la Dodoma.

 Akiwa katika eneo la Nzuguni, Naibu Katibu Mkuu, Kemikimba amekagua kazi inayoendelea ya flushing ya kisima itakayosaidia kuongeza kiasi cha maji kwa Jiji la Dodoma na amesema kuwa ameridhishwa na utendaji kazi wa  Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira  Mjini Dodoma (DUWASA) kwa kuwa wabunifu katika kutafuta vyanzo vya maji.

Ziara hizo muendelezo wa ziara zake za kukagua utekelezaji wa miradi ya maji katika Jiji la Dodoma.

Post a Comment

Previous Post Next Post