Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
amebaini ubadhilifu wa zaidi ya Bilioni 2 uliofanywa na Wakufunzi wa
Chuo Cha Ardhi Morogoro (ARIMO) na kumuelekeza Mkuu wa Chuo Huruma
Lugala kumsimamisha kazi mara moja Mkuu wa Utawala wa Chuo Michael Lori
kwa tuhuma ya kushirikiana na wakufunzi wawili wa chuo hicho
waliofanya ubadhilifu katika zoezi la urasimishaji.
Dkt
Mabula alitoa maelekezo hayo mwishoni mwa wiki mkoani Morogoro wakati
akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi pamoja na uongozi wa mkoa wa
Morogoro akiwa katika ziara yake ya siku moja kukagua utendaji kazi wa
sekta ya ardhi pamoja na miradi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la
Taifa (NHC).
Alisema,
Wizara yake ilifikiri kushirikisha makampuni binafsi katika zoezi la
urasimishaji ingerahisisha kazi ya kupima na kumilikisha wananchi maeneo
yao lakini matokeo yake baadhi ya makampuni na watu wachache wametumia
nafasi hiyo kufanya ulaghai wa kuchukua fedha za wananchi bila
kukamilisha kazi ya urasimishaji.
Kwa
mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mkuu wa
Utawala katika Chuo cha Ardhi Morogoro ameonekana kushirikiana na
watuhumiwa kwa namna moja ama nyingine na uamuzi wa kumsimamisha ni
kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.
Naye,
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emanuel Kalobelo ameeleza namna
anavyosikitishwa na baadhi ya watumishi wa sekta ya ardhi mkoani hapo
wanavyofanya Kazi na kumtia aibu katakana na utendaji wao mbovu, na
ameahidi kuwasimamia kikamilifu ili muleta ufanisi.
Awali
Dkt Mabula alielezwa na Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro Huruma Lugala
kuwa wakati uongozi wa chuo hicho ukifanya jitihada za kukiboresha chuo
ikiwemo kudhibiti hujuma mbalimbali ilibainia baadhi ya Wakufunzi wake
kujihusisha na kazi ya urasimishaji katika maeneo mbalimbali kwa kutumia
jina la chuo kujipatia fedha.
Alisema,
chuo chake baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na kubainia
udanganyifu kwa baadhi ya watumishi wake kiliamua kuwasimamisha
Wakufunzi wawili kupisha uchunguzi na kuwataja watumishi hao kuwa ni
Adolf Milungala anayetuhumiwa kujipatia shilingi Bilioni 1.9 na Hamis
Abdalah Kindemile milioni 275 fedha zilizokuwa malipo ya urasimishaji
katika mitaa 43 Morogoro.