Na Zainab Nyamka, Michuzi Tv
IFIKAPO Aprili 2021, Wakazi wa Kigamboni wanatarajia kuondokana na tatizo la maji la muda mrefu baada ya kukamilika kwa mradi wa maji wa Kigamboni. Hadi sasa jumla ya Visima 7 vimeweza kukamilika na vina uwezo wa kuzalisha maji Lita Milion 57 kwa siku.
Kwa sasa, mahitaji ya mji wa Kigamboni ni lita Milioni 25 kwa siku, na kumalizika kwa mradi huu kutawanufaisha pia wakazi wa Wilaya ya Temeke.
Bodi ya wakurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam ( DAWASA) imetembelea na kuona maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji ya Kigamboni sambamba na mradi wa Mkuranga.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi wa Dawasa Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali Davis Mwamunyange amesema hitajio la maji kwa wananchi wa Mkuranga na Kigamboni linaenda kufikia mwisho.
Amesema, kwa sasa ujenzi unaendelea katika hatua nzuri, wakandarasi wanaendelea kwa kasi na kufikia Aprili 2021 wananchi waanze kupata huduma ya maji safi.
"Mradi huu wa Visima vya Mpera na Kimbiji ni moja ya mradi mkubwa sana, utamaliza tatizo la maji Mkuranga na Kigamboni na baadhi ya maeneo ya Temeke," amesema.
Aidha, Mwamunyange amesema kukamilika kwa mradi huu kutatua pia tatizo la maji katika maeneo ya Temeke
Akielezea mradi wa Kigamboni, Afisa Mtendaji Mkuu Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema hadi sasa jumla ya visima 14 vimechimbwa vyenye urefu wa mita 400 hadi mita 600.
Amesema, kukamilika kwa visima 7 vya Kimbiji kumetoa kipaumbele kwa mradi wa majj Kigamboni kutekelezwa kwa awamu tatu na hadi kufikia Aprili 2021 wananchi wa Kigamboni watapata huduma ya maji ya uhakika.
"Mradi wa Kigamboni utatekelezwa kwa awamu tatu, moja ni kununua na kufunga pampu kwenye visima vilivyokamilika, ujenzi wa vituo vya kusukumia maji, ujenzi wa mabomba kutoka katika kisima hadi kituo cha kusukumia maji,"
Aidha, awamu ya pili ni ujenzi wa tanki lenye ujazo wa mita 15,000 eneo la Kisarawe 2, ujenzi wa kituo cha kupokelea maji na kusukumia maji kwenda katika tanki kuu, ujenzi wa bomba la kusafirishia maji Km 5.7
Katika awamu ya tatu, utakuwa ni ujenzi wa mabomba ya usambazaji maji kwa umbali wa Km 65 na uunganishaji wateja majumbani.
Ameongeza, usanifu umeanza na utakamilishwa mwezi Disemba 2020 na utanufaisha maeneo ya Kibada, Toangoma, Kigamboni, Mji Mwema, Vijibweni, Kimbiji, Kisarawe 2 na Gezaulole