TANESCO SACCOS KUJENGA JENGO LA OFISI

 


Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo TANESCO kimeanza mchakato wa shughuli za ujenzi wa jengo la ofisi baada ya kukamilika kwa taratibu za kuhamisha hati ya kiwanja kutoka Chama cha Ushirika wa Nyumba Mwenge (MHCS) kuja TANESCO SACCOS.

Akisoma Taarifa yake kwenye Mkutano Mkuu uliofanyika kwa siku mbili tarehe 14 - 15 Novemba, 2020 Jijini Dar Es Salaam, Mwenyekiti wa TANESCO SACCOS, Somoe Nguhwe amesema chama kimempata Mshauri Mwwelekezi wa mradi wa ujenzi (Consultant) ambaye ameanza kazi kwa kuandaa michoro na kuandaa nyaraka za kumpata mjenzi (Contractor).

Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, amewapongeza viongozi wa TANESCO SACCOS kwa hatua ya kuanza taratibu za ujenzi wa jengo la ofisi.

“Nichukue nafasi hii kuwasihi viongozi kuendelea na mchakato wa utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi la jengo la ofisi, ili kukuza taswira ya Chama na kuokoa gharama zinazoingiwa na Chama kulipa kodi ya pango,” amesema Dkt. Ndiege

Hata hivyo, Dkt. Ndiege amesema kuwa ujenzi huo lazima uzingatie maslahi ya wanachama na kutowafanya wanachama kukosa mikopo kwa kisingizio cha kujenga. Pia ujenzi huo ufuate kikamilifu sheria na miongozo ya manunuzi na uwekezaji kwenye vyama vya ushirika.

Mrajis amekipongeza Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo TANESCO kwa kuwa kati ya vyama vichache vilivyoweza kupata Hati Safi na kudhihirisha kuwa chama hicho kimeendelea kusimamia mali za wanachama kwa uaminifu.

Dkt. Ndiege amewapongeza viongozi na wanachama wa TANESCO SACCOS kwa hatua madhubuti wanayoichukua ya uwekezaji katika taasisi za ndani ya Sekta kwa maana uwekezaji katika ya Benki wa Ushirika (KCBL).

“Niwahakikishie kwamba serikali kupitia Benki Kuu (BoT) na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) imejipanga kusimamia benki hii muhimu kwa wanaushirika na watanzania kwa ujumla. Niwahakikishie hii ni fursa muhimu sana ya uwekezaji,” amesema Dkt. Ndiege.

Mkutano Mkuu wa TANESCO SACCOS kwa mwaka huu ni wa uchaguzi ambapo Wajumbe watachagua viongozi ambao watasimamia Chama kwa kipindi cha miaka mitatu. Dkt. Ndiege amewaasa wajumbe wa Mkutano Mkuu kuwa makini sana kuhakikisha kuwa wanachagua viongozi mahiri ambao wataendeleza kazi nzuri iliyofanywa na Uongozi unaomaliza muda wao.

“Uongozi wa Chama ndiyo Dira kwa maendeleo ya Chama kwani kama uongozi ukiwa legelege uwezekano wa kuua Chama ni mkubwa kwani wanachama watakosa imani. Hivyo kabla ya kuchagua hakikisha unatafakari usichague kwa ushabiki,” amesema Mrajis.

Kwa kuzingatia utendaji mzuri wa bodi iliyo maliza kazi yake, na Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya Mwaka 2013, Kifungu cha 137 kinampa Mrajis mamlaka ya kuteua mjumbe / wajumbe wa Bodi ambao ataona wanafaa kushika nafasi ya ujumbe huo kwa maslahi ya umma na chama kwa ujumla.

Kwa kuzingatia mamlaka haya aliyonayo Mrajis, amemteua Bi. Somoe Nguhwe ambaye atakuwa sehemu ya Bodi ya TANESCO SACCOS kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi, ubora wa huduma pamoja na kuendelea kuimarisha Sekta ya Ushirika wa Akiba na Mikopo nchini na nje ya nchi. Aidha, Lengo kubwa ni kuendeleza ushirikiano kwenye taasisi zetu za Ushirika nchini (SCCULT) pamoja na ushirikiano wa nje ya nchi (ACCOSCA na WOCCU).

Bi. Somoe Nguhwe amekuwa mwanachama mwenye uzoefu mkubwa na amesomea na kufanya kazi za masuala ya ushirika kwa kipindi kirefu tangu Mwaka 1984. Mwanachama huyu amekuwa na uzoefu kwenye nafasi ya uongozi na utendaji kazi kwenye SACCOS tangu Mwaka 1981.

Dkt. Ndiege amesema kuwa Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania imedhamiria kuimarisha utendaji kazi wa Vyama vya Ushirika nchini ikiwa ni pamoja na kuendelea kuweka taswira nzuri ya Ushirika kwa umma ili wananchi wengi waweze kuvutiwa na kuendelea kutumia huduma na bidhaa zinazotolewa na Vyama vya Ushirika nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post