MALISA AITAKA TFRA KUHAKIKISHA WAKULIMA WANAPATA MBOLEA KWA WAKATI

Mwandishi Wetu,

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa, ameielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuendelea kuhakikisha wakulima wanapata mbolea ya kutosha na kwa wakati ili kuwawezesha kujiandaa mapema kwa msimu ujao wa kilimo.

Mhe. Malisa ametoa maelekezo hayo leo wakati akifungua rasmi Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Mwakangale, jijini Mbeya, ambapo amesisitiza umuhimu wa upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa wakati ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao.

Akizungumzia hali ya upatikanaji wa mbolea nchini, Meneja wa TFRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Joshua Ng’odya, amesema wakulima hawana sababu ya kuwa na wasiwasi kwani mbolea ipo ya kutosha na mipango imewekwa kuhakikisha inawafikia kwa wakati.

Ng’odya amesema kwa sasa nchini kuna tani 248,617 za mbolea zilizopo katika maghala mbalimbali, huku tani 313,800 zikitarajiwa kuingia nchini katika kipindi kifupi kijacho ili kuendelea kuimarisha upatikanaji wa mbolea kuelekea msimu wa kilimo.

Aidha, amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027, TFRA imelenga kuratibu upatikanaji wa tani 1,500,000 za mbolea nchini, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha hakuna mkulima anayekosa pembejeo hiyo muhimu.

Amewahimiza wakulima kujiandaa mapema kwa msimu wa kilimo, kununua mbolea kutoka kwa wauzaji waliosajiliwa na kutumia mbolea kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa kilimo ili kuongeza uzalishaji na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


Post a Comment

Previous Post Next Post