Mwandishi Wetu,
Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati Jijini Dodoma yaliyoanza tarehe 1 Agosti 2026 baada ya yakifunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba yameendelea kuvuta wageni wengi kutembelea banda la wizara ya Maliasili na utalii na kushuhudia vivutio mubashara kutoka Ngorongoro kupitia luninga kubwa iliyofungwa Katika viwanja hivyo.
Wageni waliotembelea banda hilo ni pamoja Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena, Brigedia Jenerali Shija Lupi, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT) na wananchi mbalimbali ambao wameelezwa vivutio mbalimbali vya wanyamapori, malikale na urithi wa utamaduni unaoelezea historia ya binadamu katika hifadhi ya Ngorongoro
Mhe. Waziri Kijaji alipotembelea banda hilo ameeleza kuwa “Nawapongeza Ngorongoro kwa jitihada za kutumia mifumo ya kidigitali kutangaza vivutio vya utalii, tumeeleza uwepo wa vivutio mbalimbali vya wanyamapori, milima, uwepo wa Kreta tatu, mchanga unaohama, mazalia ya nyumbu, maporomoko ya maji na vingine vingi vinavyoashiria kuwa Ngorongoro ni Nyumbani kwa kila kivutio”
Kwa upande wake Brigedia Jenerali Shija Lupi amesema kuwa kuona vivutio mubashara vya utalii katika maonesho ya nanenane na kuelezwa hadithi za chimbuko la binadamu na gunduzi za visukuku mbalimbali, nyayo za Laetoli na ugunduzi wa Fuvu la Zinjanthropus vinaashiria kuwa kila binadamu asili yake ni Ngorongoro na kuonyesha umuhimu wa kutembelea hifadhi hiyo
Brigedia Shija ameongeza kuwa kutumia teknolojia katika maeneo ya hifadhi ina mchango mkubwa wa kutangaza vivutio vya utalii duniani na kuimarisha ulinzi kwa rasilimali za nchi.


