WASHIRIKI zaidi ya 2500 kutoka mataifa mbalimbali duniani wanatarajia kushiriki Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Huduma ya Afya ya Msingi utakaofanyika Septemba 9 hadi 11, 2026 jijini Arusha.
Katika mkutano huo machapisho zaidi ya 400 yanayohusu masuala ya afya yatajadiliwa ili kupata njia ya pamoja kufanikisha utoaji huduma bora ya afya ya msingi huku Tanzania ikiendelea kujitangaza kuwa kinara katika ufanisi wa mpango huo.
Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi, Dkt Rashid Mfaume, ametanabaisha hayo leo jijini Dar es Salaam na kufafanua kwamba miongoni mwa wadau watakaokuwemo katika mkutano huo ni wabunifu wa teknolojia wa huduma za Afya.
Wengine ni watafiti katika nyanja ya afya, wadau mbalimbali wa maendeleo, watunga sera, vyuo vikuu mbalimbali vya ndani na nje ya nchi jambo litakalosaidia kuiweka Tanzania katika ramani bora ya utoaji huduma hiyo.
Aidha wageni mbalimbali wataofika katika mkutano huo wataweza kubadilishana uzoefu katika nyanja hiyo na namna Tanzania ilivyoweza kufanikiwa katika utoaji huduma ya msingi kwa wananachi kuanzia ngazi ya Zahanati.
Tunafanya mkutano huu kwa mara ya pili ili kuhamasisha jamii na kuongeza uelewa kuhusu huduma za afya ya msingi ambayo ni muhimili katika kuleta maendeleo ya taifa lolote hasa kwenye ujenzi wa afya za wananchi.
Naye Dkt. Pius Kagoma amesema katika nyanja ya afya ikibaki salama pia mataifa mengine yatakuwa salama, hivyo dunia lazima ifahamu kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta hiyo na itawezeza mataifa mengine kujifunza ili kufanikisha mpango huo.
Pia aliongeza kuwa licha ya mambo mengine maandalizi yanaendelea kukamilika, pia kupitia mkutano huo wataishirikisha Wizara ya Utalii ili kutangaza vivutio mbalimbali vilivyopo Tanzania.



