Mwandishi Wetu,
Mradi wa huduma ya majisafi wa Kwamaizi umekamilika kwa gharama ya Shilingi milioni 465,182,915.20 na utanufaisha zaidi ya wakazi elfu sita wa Handeni Mkoani Tanga.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amepokea mradi huo na kusema Serikali itaendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji safi, usafi wa mazingira ili kuboresha afya na ustawi wa jamii.
Ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Handeni (HTM), RUWASA, viongozi wa Serikali za Mitaa na wananchi kuendelea kulinda, kutunza na kusimamia miundombinu ya huduma ya maji ili huduma hiyo iendelee kuwa endelevu na kuwanufaisha wananchi kwa muda mrefu.
Naye Mkurugenzi Mkazi wa asasi ya WaterAid Tanzania, Bi. Anna Mzinga, amezitaka taasisi hizo kuweka mikakati madhubuti ya kuendeleza na kupanua huduma za mradi huo ili kuwafikia wanufaika wengi zaidi.
Mradi wa Kwamaizi umetekelezwa na asasi ya WaterAid Tanzania kwa ufadhili wa OKF, kwa kushirikiana na Wizara ya Maji na Halmashauri ya mji wa Handeni.
Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa chujio la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo laki moja, tenki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita laki moja, ulazaji wa bomba kuu la kusafirisha maji lenye urefu wa mita 1,485, uchimbaji na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji yenye urefu wa mita 2,358, pamoja na ujenzi wa vituo vitatu vya umma kucha maji vyenye mfumo wa malipo ya kabla.
Mradi utanufaisha wananchi wa maeneo ya Kideleko, Kampene, Muungano, Ndekai na Bangu.
















