Imeelezwa kuwa, zao la ufuta ni miongoni mwa mazao yanayohitaji matumizi makubwa na sahihi ya mbolea ili kuongeza tija ya uzalishaji na kuboresha ubora wa mavuno.
Mtaalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ametoa maelezo hayo mbele ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent, alipotembelea banda hilo katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Amebainisha kuwa, wakulima wengi wa kusini mwa Tanzania hufanya kilimo cha kuhamahama kutafuta maeneo yenye rutuba badala ya kutumia mbolea kutokana na mazoea ambapo wakitumia mbolea kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu wataongeza uzalishaji wa zao hilo pamoja na kuongeza thamani yake bila kuadhiri eneo la makuzi ya watoto kutokanako na kuhamahama.
Akizungumza baada ya kutembelea mabanda ya taasisi mbalimbali yaliyoshiriki maonesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji, Laurent, amesema ushirikiano miongoni mwa taasisi za utafiti, sekta binafsi na wadau wa kilimo ni msingi muhimu katika kuimarisha matumizi sahihi ya mbolea, kuongeza uwekezaji na kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Laurent amesema TFRA itaendelea kushirikiana na TARI katika kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya kimkakati, ikiwemo ufuta.
Katika banda la Sustainable Agriculture Tanzania (SAT), Meneja wa Mradi wa taasisi hiyo, Peter Mwangalo, amemueleza Laurent kuhusu juhudi zinazofanywa katika kuhamasisha kilimo endelevu na matumizi ya mbolea za asili.
Akiwa ndani ya banda la TPHPA, Laurent ameelezwa tofauti kati ya mbolea za maji na viuatilifu kuwa, mbolea hutoa virutubisho vinavyohitajika kwa ukuaji wa mimea, wakati viuatilifu ni sumu iliyoandaliwa maalum kwa ajili ya kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao.
Pamoja na mabanda hayo, Laurent ametembelea banda la Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC),Tume ya Maendeleo ya Ushirika ikiwa ni sehemu ya juhudi za TFRA za kuimarisha ushirikiano na wadau wa tasnia.




