RAIS SAMIA AFUNGUA MKUTANO WA MAWAKILI WA SERIKALI, ASISITIZA WELEDI, UADILIFU NA ULINZI WA RASILIMALI ZA TAIFA

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Mawakili wa Serikali kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu, weledi, uzalendo mkubwa na kuwa walinzi wa rasilimali za taifa kwa kutumia kalamu na sheria.

Rais Samia ameyasema hayo, wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali, tarehe 13 Julai, 2026 Jijini Arusha .

“Nataka nilisisitize hilo, Kalamu ya Mwanasheria ikitumika vizuri inaweza kuzuia hasara kabla haijatokea, inaweza kulinda mkataba kabla haujawa mzigo kwa serikali, na inaweza kuiongoza Serikali kufanya maamuzi bora na yenye maslahi kwa taifa.” Amesema dkt. Samia

Aidha, Dkt Samia amewataka Mwakili wa Serikali kuendelea kuwa walinzi wa rasilimali za taifa kwa kutoa ushauri wa kisheria kwa usahihi, uzalendo, uaminifu na kutanguliza mbele maslahi ya taifa ambapo Serikali itaendelea kuwawezesha Mawakili wa Serikali kwa kuwajengea wa kitaaluma na Mazingira wezeshi ya kazi zao.

Katika hatua nyingine, Mhe, Rais ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua mbalimbali ambazo Ofisi inaendelea kuzichukua katika kuimarisha mifumo ya upekuzi wa mikataba, urekebu wa tafsiri ya sheria, msaada wa kisheria, Kliniki ya Sheria na mafunzo na elimu ya Sheria kwa Wananchi.

“Nawapongeza sana kwa hatua hizi za kuimarisha mifumo ya mikataba, urekebu wa tafsiri za sheria, Msaada wa kisheria na Kliniki za sheria, hatua hizi kwa njia moja au nyingine zimesaidia kuimarisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo na ustawi wa wananchi wetu.” Amesema Mhe. Rais

Vilevile. Dkt. Samia amepongeza jitihada za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuendeleza huduma za msaada wa kisheria ikiwezo kazi ya kutafsiri sheria kwa lugha ya Kiswahili ambayo iko mbioni kakamilika.

“Hatua hii mliyoichukua ni muhimu na ya kupongezwa kwani mwananchi anapoielewa sheria anaelewa haki zake, wajibu wake, mipaka ya uhuru wake na mipaka ya mamlaka ya Serikali hii ndio maana halisi ya utawala wa Sheria. Amesema Mhe. Rais.

Dkt. Samia ameeleza kuwa, ili kufikia malengo ya Dira ya Tafia ya 2050 ni lazima kuwa na mfumo wa Sheria unaoshawishi wananchi kujielekeza na kuchangia kwenye Uchumi imara, Shindani, jumuishi na unaongozwa na maarifa na ubunifu.

“Mwelekeo wa Taifa hili kwa miaka 25 ijayo ni kuona mfumo wetu wa sheria na utoaji wa haki unashawishi watu kujielekeza na kuchangia kwenye Uchumi imara, Shindani, jumuishi na unaongozwa na maarifa na ubunifu, hili litawezekana tukiwa na sheria bora.”

Amesema Dkt. Samia

Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera ameeleza kuwa Wizara ya Katiba na Sheria inaendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na Chama cha Mawakili wa Serikali kupitia mlezi wa Chama hicho, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambapo Wizara imeweza kukipatia chama hicho Ofisi katika jengo la Wizara lililoko Mtumba Jijini, Dodoma.

Naye, Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali anayemaliza muda wake, Bw. Bavoo Junus amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali yake ya Awamu Sita kwa kukiwezesha Chama cha Mawakili wa Serikali kutekeleza majukumu yake kwa usahihi, na kukifanya chama hicho kuendelea kukua na kuimarika huku kikitoa mchango chanya, tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Mawakili wa Serikali.

Aidha, Bw. Bavoo ameeleza kuwa chama hicho kitaendelea kushiriki katika programu za utoaji wa huduma za msaada wa kisheria katika mikoa mbalimbali na kuhakikisha wananchi wanapata elimu kuhusiana na masuala mbalimbali ya kisheria.

Mkutano Mkuu wa Chama cha Mawakili wa Serikali uliofunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 13 Julai, 2026, Pamoja na mambo mengine utahusisha Uchaguzi wa nafasi mbalimbali za uongozi katika chama hicho unaotarajiwa kufanyika tarehe 14 Julai, 2026.

Post a Comment

Previous Post Next Post