Mwandishi Wetu Mbeya,
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imepongezwa kwa mchango wake mkubwa katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira kupitia utekelezaji wa miradi ya ujenzi na matengenezo ya barabara, madaraja na vivuko katika maeneo mbalimbali nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya TARURA, Bw. Henry Kaywanga wakati akihitimisha ziara ya ukaguzi wa miradi ya Wakala huo mkoani Mbeya.
Amesema miradi inayotekelezwa na TARURA imekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi kwa kutoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja huku ikichochea shughuli za kiuchumi na kuongeza thamani ya maeneo yanayofikiwa na miundombinu hiyo.
"Miradi hii siyo tu inaboresha miundombinu ya usafiri bali pia inafungua fursa za ajira, inaongeza thamani ya maeneo na kurahisisha shughuli za kila siku za wananchi. Huu ni mchango muhimu katika kukuza uchumi wa maeneo husika na taifa kwa ujumla", amesema Bw. Kaywanga.
Aidha, Kamati hiyo imeishauri TARURA kuendelea kuwa makini katika usimamizi wa makandarasi ili kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaokidhi viwango vilivyowekwa na kutoa thamani halisi ya fedha za umma.
Naye, Mjumbe wa Kamati ya Ukaguzi, Mhandisi Sylivester Ahonga amesisitiza umuhimu wa kufanya maandalizi ya kina kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza ikiwemo changamoto za mvua na mazingira mengine yanayoweza kuchelewesha kazi.
Pia amewataka watendaji wa TARURA kuendelea kuzingatia misingi ya uadilifu, uwajibikaji na usimamizi madhubuti wa mikataba ili miradi yote ikamilike kwa wakati na kwa ubora unaotarajiwa na kuendelea kuwanufaisha wananchi pamoja na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.






