Mwandishi Wetu,
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imewakumbusha wamiliki na madereva wa magari ya utalii kuwa makini , kuhakikisha magari yao yapo salama na kuzingatia sheria na taratibu za maeneo ya hifadhi hasa katika kipindi hiki cha msimu mkubwa wa utalii (High Season).
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka hiyo imeeleza kuwa ni muhimu madereva na wamiliki wa magari ya kubeba watalii kuhakikisha wanatengeneza magari hayo ipasavyo, kuyakagua mara kwa mara na kuwa na madereva makini na wenye weledi wa kutosha wanapoendesha magari hayo..
“Tumeanza msimu mpya wa utalii, tunawakumbusha na kuwasisitiza wadau wote katika mnyororo wa utalii kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha usalama wa watalii na watumiaji wengine wa barabara katika maeneo ya hifadhi unakuwa wa uhakika”,ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uongozi wa Hifadhi ya Ngorongoro umejipanga kuendelea kutoa huduma zote muhimu kwa kuzingatia ubora na wakati sambamba na kutoa elimu ya mara kwa mara kwa madereva wa magari yanayobeba watalii na magari yanayobeba watu wengine wanaoishi ndani ya hifadhi kwa lengo la kuhakikisha usalama wa kila mtu unalindwa.
Uzoefu unaonesha kuwa katika msimu wa watalii wengi baadhi ya kampuni hutumia magari yasiyokuwa na ubora na baadhi ya madereva kutokuwa na uzoefu wa kutosha kuendesha watalii hifadhini hali inayosababisha changamoto kwa Watalii.
