Waziri wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji (Mb), ameongoza kikao kazi cha maandalizi ya bajeti ya Wizara hiyo inayotarajiwa kuwasilishwa katika Bunge la bajeti la mwaka wa fedha 2026/2027 linaloendelea Jijini Dodoma.
Dkt. Kijaji anatarajiwa kuwasilisha Bungeni Mpango na Makadirio ya mapato na matumizi ya wizara pamoja na Taasisi zake jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Kijaji amesisitiza kuwa ni muhimu kwa Wizara kuhakikisha bajeti yake inaakisi mahitaji halisi ya wananchi na kuendana na matarajio yao.
“Ni muhimu sana kuwa na hisia za wananchi wetu, hasa kujua wanahitaji nini na sisi tujipange vipi ili kufikia malengo yao. Hii ina maana kuwa na hotuba ya bajeti yenye jicho la wananchi,” amesema Dkt. Kijaji.
Aidha, amezitaka Taasisi, Idara na Vitengo zilizo chini ya wizara hiyo kuwasilisha mambo matatu makubwa waliyotekeleza kwa mafanikio katika mwaka wa fedha 2025/26, pamoja na kuainisha vipaumbele vitatu kwa mwaka 2026/27 vitakavyowanufaisha wananchi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, amesema kikao hicho ni sehemu ya maandalizi muhimu ya bajeti, yakilenga kuweka mikakati madhubuti ya kukuza sekta ya uhifadhi, maliasili na utalii ili kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa.














