MAHUNDI: SERIKALI KUENDELEA KUIMARISHA VIKUNDI NA MIKOPO KWA WANAWAKE

 

Na Jackline Minja, WMJJWM-Dodoma

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema Serikali inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha vikundi vya wanawake kiuchumi pamoja na kuboresha upatikanaji wa mikopo nafuu ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

Akijibu swali bungeni kuhusu uwezeshaji wa vikundi na mikopo kwa wanawake, Mahundi amesema Serikali inashirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali ikiwemo mashirika binafsi na benki ili kuhakikisha wanawake wanapata fursa pana zaidi za kifedha.Amesema ushirikiano huo umewezesha upatikanaji wa mikopo nafuu kwa makundi mbalimbali ikiwemo vijana wa bodaboda, huku akisisitiza kuwa elimu na taarifa sahihi kuhusu mikopo hiyo zinaendelea kutolewa kupitia maafisa Maendeleo ya Jamii ili kuwafikia walengwa kwa ufanisi zaidi.

“Serikali imeweka mazingira rafiki ya utoaji wa mikopo kwa kuondoa vikwazo visivyo vya lazima na kuboresha masharti ili kuhakikisha kila mwenye uhitaji anapata mkopo kwa urahisi na kwa wakati,” amesema Mahundi.Aidha, ameeleza kuwa pamoja na kurahisisha masharti, Serikali imeendelea kusimamia utoaji wa mikopo hiyo kwa umakini ili kuhakikisha inawanufaisha walengwa waliokusudiwa na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika jamii.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amewataka wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kutokwamisha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Serikali, akisisitiza kuwa fedha hizo ni maelekezo mahsusi ya Serikali kwa ajili ya kuwainua wananchi kiuchumi.

“Ni wajibu wa wakurugenzi kuhakikisha mikopo ya asilimia 10 inatolewa kwa wakati na kwa walengwa sahihi ili kufikia dhamira ya Serikali ya kupunguza umasikini miongoni mwa wananchi,” amesisitiza.

Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mpango huo ili kuhakikisha unaleta matokeo chanya kwa wananchi, hususan wanawake na vijana wanaotegemewa kuwa chachu ya maendeleo ya taifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post