LENGO LETU NI KUREJESHA TABASAMU KWA WANANCHI- MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI

 

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari ameshiriki hafla ya kukabidhi magari kwa Kampuni ya SEMA Limited iliyofanyika katika Viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, tarehe 22 Aprili, 2026.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa, zoezi hilo la kukabidhi magari ni matokeo ya Kliniki ya Kisheria bila malipo iliyofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 25 Aprili, 2025 katika Viwanja vya Stendi ya zamani Manispaa ya Singida, Mkoa wa Singida.

Aidha, Mhe. Johari ameeleza kuwa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilipokea lalamiko la Bw. Lameck Muyanzi (Meneja wa Karakana wa Sustainable Environment Management Action (SEMA) aliyelalamikia Kampuni ya TAOMTRA Limited (Hussein Mjili na Getruda Agripa Mwashambwa - Dalali wa Mahakama) kwa kukamata magari matano (5) ya Kampuni ya SEMA na kuyauza magari husika isivyo halali.

“Tulipokea lalamiko kutoka Kampuni ya SEMA na nilikabidhi kwa watalaamu kwa ajili ya kulishughulikia na matokeo yake ndio haya mnayaona leo hapa.” Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amesema kuwa Ofisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Upelelezi Mkoa wa Singida pamoja na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Singida, ilifanya jitihada za kuyarejesha magari hayo kwa kampuni ya SEMA.

“Dhumuni kubwa la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni kutatua changamoto za wananchi katika hali ya kawaida ili kuipinguzia Mahakama mzigo.” Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Vilevile, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea na utaratibu wa kutembelea maeneo mbalimbali nchini na kutatua kero mbalimbali za kisheria zinazowakabili wananchi.

“Tutaendelea kuwasaidia wananchi kutatua kero zao za kisheria na kuwarejeshea tabasamu wananchi kama alivyoagiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.” Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe. Godwin Gongwe amempongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili wananchi hususani wa Mkoa wa Singida.

“Tunakupongeza sana Mhe. Hamza Johari kwa kazi kubwa unayoifanya sisi Singida tunakuona kama ni Alama ya Haki. Amesema Mhe. Gondwe

Awali akitoa neno la utangulizi Mkurugenzi wa Divisheni ya Uratibu na Ushauri wa Kisheria Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bi. Neema J. Ringo amezishukuru Taasisi mbalimbali zilizoshiriki katika kushughulikia lalamiko hilo na kuweza kulitatua na kuwezesha Kampuni ya SEMA kurejeshewa magari yaliyokuwa yameshikiliwa na Kampuni ya TAOMTRA Limited.

“Tunavishukuru vyombo mbalimbali vya Serikali vilivyohusika katika kutatua suala hili, Serikali ilifanya kazi kama timu na mafanikio tumeyaona.” Amesema Bi. Ringo

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya SEMA Bw. Ivo Manyako amemshuruku Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Watendaji wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushugulikia changamoto iliyokuwa inawakabili na kufanikisha kurejeshewa magari ya Kampuni ya SEMA yaliyokuwa yanashikiliwa na Kampuni ya TAOMTRA Limited.

“Kwa niaba ya Kampuni ya SEMA tunakushukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kulibeba suala hili na kulitatua kwa Weledi, na pengine kwa Weledi huo ndio uliomfanya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu kukuteua tena kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” Amesema Bw. Manyako

Kampuni ya SEMA Limited imefanikiwa kurejeshewa jumla ya magari manne (4) ambayo ni Toyota Land Cruiser S/Wagon lenye namba za usajili T465 AED; Isuzu Winch lenye namba za usajili T418 AED; Isuzu Tipa lenye namba za usajili T423 AED na Land Rover 101 Station Wagon lenye namba za usajili T412 AED. Aidha, walalamikiwa walitakiwa kulipa kiasi cha Shilingi 27,750,000 kufidia gari moja lililokuwa limeharibiwa.

Post a Comment

Previous Post Next Post