Na OWM-TAMISEMI, Mwanza
Imefahamishwa kuwa Mradi wa Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) unaotekelezwa katika mikoa 11 nchini umeanza kuonesha mafanikio makubwa kutokana na ongezeko la uzalishaji kupitia mafunzo ya mashamba darasa.
Mafanikio hayo yamebainishwa na Mratibu Msaidizi wa mradi huo, Bw. Theodori Mulokozi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), mara baada ya kufanya tathmini kwa wakulima walioshiriki kikamilifu katika mafunzo hayo na kuyatekeleza kwa vitendo.
“Wapo wakulima ambao sambamba na kushiriki katika mafunzo haya kupitia vikundi, walienda kulima katika maeneo yao binafsi. Tumeona wakishukuru kwa sababu wamepata mavuno mengi na haya ndio matokeo halisi ya programu yetu; kuongeza uzalishaji wenye tija na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja,” amesema Bw. Mulokozi.
Ameeleza kuwa wakulima hao walipata mafunzo kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa kilimo mwezi Oktoba 2025, ambapo walipatiwa mbegu na mbolea bure pamoja na ushauri wa kitaalamu. Kupitia mashamba darasa, walilima mazao ya mahindi, alizeti na mikunde chini ya usimamizi wa maafisa ugani katika Kata husika.
Kwa upande wake, mkulima kutoka Kata ya Misasi, Wilaya ya Misungwi, Bw. Nkwambi Piusi Manonga, amesema elimu hiyo imeleta mabadiliko makubwa katika uzalishaji wake.
“Mimi ninashukuru elimu hii imenisaidia. Zamani nilikuwa napata magunia 15 ya mahindi katika hekari nne, lakini mwaka jana nimelima hekari mbili tu na kupata magunia 30,” amesema Bw. Manonga.
Naye Afisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Innocent Keya, amesema mradi huo unatekelezwa katika wilaya za Kwimba, Misungwi na Sengerema, ambapo jumla ya kata 15 zinashiriki.
“Wakulima wamenufaika na elimu ya kilimo cha mahindi, alizeti na mikunde, jambo lililoongeza uzalishaji na kipato chao,” amesema Bw. Keya, huku akiwahimiza wakulima kuendelea kusambaza maarifa hayo kwa wengine.
Mradi wa AFDP unatekelezwa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na wadau wa maendeleo, ukiwemo Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD). 


