Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeendelea kuimarisha mikakati yake ya kuhakikisha usalama na huduma bora kwa watalii wanaotembelea hifadhi zake, hususan maeneo ya milima kama Kilimanjaro na Udzungwa.
Hatua hiyo imebainika wakati wa ufunguzi wa mafunzo maalum ya uokoaji, uhokozi na huduma ya kwanza kwa askari wa hifadhi, yaliyolenga kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazoweza kuwakumba watalii wakiwa safarini.
Akifungua mafunzo hayo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Kanda ya Mashariki, Fredrick Malisa, amesema TANAPA inaendelea kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa askari wake ili kuhakikisha wanakuwa tayari kukabiliana na hali yoyote ya dharura.
Amesema hifadhi za milima hupokea watalii wa aina mbalimbali wenye uwezo tofauti, hivyo ni muhimu kuwa na kikosi chenye ujuzi wa kuwahudumia haraka na kwa ufanisi bila kuongeza madhara kwa wahusika.
Kwa upande wake, Afisa Mhifadhi Mkuu kutoka hifadhi ya mlima kilimanjaro Miraji Mramba amesema askari kutoka Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro wamefanya mafunzo hayo katika Hifadhi ya Taifa Udzungwa kwa lengo la kujifunza katika mazingira tofauti na kuongeza ufanisi wa kazi zao.
Amesema utaratibu huo wa mafunzo hufanyika kila mwaka, hasa wakati wa msimu wa watalii wachache, ili kujiandaa na msimu mkubwa wa wageni, huku akibainisha kuwa TANAPA itaendelea kusambaza elimu hiyo katika hifadhi nyingine zenye milima nchini.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Utalii katika Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa, Ahmed Nasori, amesema ujio wa mafunzo hayo ni fursa muhimu kwa askari wa hifadhi hiyo kujifunza na kubadilishana uzoefu na wenzao wa Kilimanjaro.
Amesema mazingira ya Udzungwa yanafanana kwa kiasi kikubwa na yale ya Kilimanjaro, hivyo mafunzo hayo yataongeza uelewa wa namna bora ya kukabiliana na changamoto za uokoaji katika maeneo ya milima.
Aliongeza kuwa hifadhi hiyo pia imekuwa kivutio kikubwa cha utalii, ikitoa fursa za shughuli mbalimbali kama kupanda milima, matembezi ya asili (hiking) na utalii wa picha, huku idadi ya watalii ikiendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.




