Masauni awaonya wanaochafua mazingira

 

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Rais; Muungano na Mazingira, Hamad Yusuf Masauni, amesema Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linatakiwa kupatiwa vitendea kazi vya kisasa kama helkopta pamoja na drones kwaajili ya kufanikisha utendaji kazi wao.

Masauni amesema hayo leo machi 30, 2026, katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kuondoa taka (Taka Sifuri) ambayo kitaifa yamefanyika katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na wadau wa mazingira, huku akitoa onyo kali kwa wanaochafua mazingira wakiwemo wazalishaji mifuko ya plastiki, wanaotupa taka hovyo, kumwaga maji machafu baharini na wanaosababisha kelele mitaani na kwamba watachukuliwa hatua.

Amesema serikali inatarajia kufanya mabadiliko ya sheria kwa kuipa mamlaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ili iweze kushughulika na watakaokiuka sheria za utunzaji wa mazingira bila kujali sekta binafsi au za serikali.

“Nitashangaa sana nikija Dar es Salaam kwenye jiji la biashara liko chafu, nitasikitika sana nikikuta taasisi yoyote iwe ya serikali, iwe binafsi inazembea katika kutekeleza sheria za mazingira au haitumii fursa za kubadilisha taka kuwa fursa”

Aidha, Masauni amewataka wananchi kuchukulia maonesho hayo msingi mkuu wa kujifunza jinsi ya kubadilisha taka kuwa fursa kwaajili ya kujiongezea kipato na kuongeza uchumi wa nchi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema, mkoa wa dar es salaam imeanza mpango wa kuanza kufundisha somo la uhifadhi wa mazingira kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, na kwamba tayari shule 10 zimeshachaguliwa kwaajili ya mpango huo.

Mpogolo amesema serikali ya mkoa wa Dar es salaam kwa kushirikiana na NEMC wataanza kutoa mafunzo kwa makampuni na wakandarasi wanaohusika na kuzoa taka ili uchakataji wa taka uanze kwenye chanzo cha taka.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Immaculate Semesi, amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na urejelezi wa taka, huku akisisitiza umuhimu wa kuona taka kama rasilimali badala ya uchafu.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post