SHULE 19 ZAPATA VIFAA VYA TEHAMA

 

SHULE 19 za msingi na sekondari katika mikoa tisa nchini zimepokea vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya Shilingi milioni 769, hatua inayotarajiwa kuboresha ufundishaji wa masomo ya sayansi na teknolojia pamoja na kuongeza uelewa wa wanafunzi kupitia ujifunzaji wa vitendo.

Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa vifaa hivyo leo, Machi 30, 2026, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, alisema vifaa hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali katika elimu, kwa lengo la kuongeza ubora na ufanisi wa ujifunzaji.

Amebainisha kuwa kupitia uwekezaji huo, walimu watanufaika kwa kutumia mbinu bunifu za kufundishia, huku wanafunzi wakipata fursa ya kujifunza kwa kuona na kufanya, jambo litakalosaidia kukuza ubunifu, ujuzi wa TEHAMA na kuendana na mahitaji ya soko la ajira la sasa. “Leo tumegawa vifaa hivi; niombe visifungiwe kabatini. Vitunzeni na vitumike kwa muda mrefu ili viwanufaishe wanafunzi wengi,” alisisitiza Ameir.

Mbali na ugawaji huo, Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya elimu ya kidijitali kwa kuanzisha madarasa janja matano na kufunga mbao janja 422 katika shule za sekondari, sambamba na utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa matumizi ya TEHAMA na Akili Unde (AI) katika elimu.

Post a Comment

Previous Post Next Post