
KATIBUMkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea kuimarisha sekta ya elimu nchini kupitia matumizi ya teknolojia za kidijitali.
Akizungumza leo Machi 30, 2026, jijini Dodoma wakati wa hafla ya ugawaji wa vifaa vya kidijitali kwa shule za msingi na sekondari, Prof. Nombo amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha walimu na wanafunzi wanapata nyenzo bora za kufundishia na kujifunzia zitakazowawezesha kumudu ujuzi wa karne ya 21.
“Ugawaji huu wa vifaa ni ushahidi wa dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Tupo katika enzi ya mapinduzi ya sayansi na teknolojia, hivyo jamii haiwezi kubaki nyuma katika maendeleo haya,” alisema Prof. Nombo.

Vifaa vilivyogawiwa vinajumuisha madarasa janja, mbao janja, vishikwambi na kompyuta vyote vikilenga kuongeza ufanisi wa ufundishaji na ujifunzaji, hususan katika masomo ya sayansi na teknolojia. Aidha, Prof. Nombo amesisitiza umuhimu wa kusawazisha matumizi ya teknolojia na mbinu za jadi kama vitabu na madaftari, ili wanafunzi wapate ujuzi wa msingi sambamba na ujuzi wa kidijitali.
Pia amebainisha kuwa Mkakati wa Kitaifa wa matumizi ya teknolojia za kidijitali katika elimu unaendelea kutekelezwa kwa lengo la kujenga mfumo wa elimu ulio bora, jumuishi na endelevu. Amewataka walimu, wanafunzi na wadau wa elimu kutumia na kutunza vifaa hivyo ipasavyo ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.