Mwandishi Wetu,
Kamishna Mkuu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda mezindua jukwaa la wanawake na kodi leo tarehe 6 Februari, 2026 linalokwenda kufanya kazi ya kuwezesha biashara za wanawake kwa kutoa elimu ya kodi, kuwasikiliza na kutatua changamoto zao.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Kamishna Mkuu Mwenda amesema jukwaa hilo litakuwa kiungo baina ya TRA na wanawake.
Amesema jukwaa hilo pia linalenga kuwawezesha wanawake katika shughuli zao za biashara kupitia njia mbalimbali ikiwemo kutatua changamoto za kikodi zilizo ndani ya uwezo wa TRA, ili waweze kuendelea na shughuli zao za kibiashara bila vikwazo na kuwezesha wale ambao biashara zao zimekufa kufufuuka na kuendelea kufanya kazi.
Ameeleza kuwa TRA ni mdau mkubwa wa biashara nchini na ina jukumu la kuwa daraja kati ya wafanyabiashara na taasisi nyingine, hivyo mamlaka hiyo itaendelea kuwawezesha wafanyabiashara kufikia fursa na huduma mbalimbali muhimu kwa maendeleo ya biashara zao.
Kamishna Mkuu amesema jukkwaa la wanawake na kodi pia litasaidia katika kuwaunganisha wafanyabiashara wanawake na masoko, akibainisha kuwa changamoto kubwa inayokabili biashara ndogondogo na za kati ni upatikanaji wa masoko ya bidhaa na huduma zao.
Awali akizungumza kuhusu jukwaa hillo Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano Bw. Richard Kayombo amesema jukwaa hilo litawezesha kutolewa kwa elimu ya koodi kwa lugha rahisi, kujenga uhusiiano na Walipakodi na kutatua changamoto zao. 



