Kuelekea siku ya wanawake duniani :TFRA yatoa mafunzo kwa wakulima wa mbogamboga

Mwandishi Wetu,

Wakulima wa mbogamboga katika maeneo ya TAZARA na Kata ya Mtoni,  wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam, wamepatiwa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji, ikiwa ni sehemu ya  kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Akizungumza leo Machi 3, 2025, wakati wa mafunzo hayo, Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi Gema Nganyangwa kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) amesema mamlaka inatambua mchango mkubwa wa wakulima wadogo, hususan wanawake, katika uzalishaji wa mbogamboga na kuimarisha usalama wa chakula. Amesema ni muhimu kuwafikia moja kwa moja na kuwapatia elimu ya matumizi sahihi ya mbolea pamoja na kuwafahamisha fursa mbalimbali zilizopo katika tansnia ya mbolea.

Nganyangwa amesisitiza umuhimu wa wakulima kuepuka kununua mbolea za kupima, akieleza kuwa mara nyingi hupoteza ubora na virutubisho pale zinapofunguliwa na kuhifadhiwa visivyo sahihi. Amewahimiza kununua mbolea zilizosajiliwa na kuidhinishwa ili kupata matokeo bora shambani.

Naye Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Temeke, Bi. Anna Kasege, ameishukuru TFRA kwa kuwafikia wakulima wa Temeke, wengi wao wakiwa wanawake, na kuwapatia elimu itakayowawezesha kuongeza mavuno hata katika maeneo madogo wanayolima.

Aidha, Bi. Kasege amewahimiza wakulima kujisajili ili waweze kunufaika na mpango wa mbolea ya ruzuku kwa bei elekezi, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa pembejeo bora na kuongeza tija katika uzalishaji.

Kwa upande wake, Bi. Suzan Jalala, mkulima wa mbogamboga katika eneo hilo, ameishukuru mamlaka kwa elimu waliyoipata, akisema imewasaidia kuelewa umuhimu wa kutumia mbolea zilizo bora na kuepuka mbolea za kupima ambazo hupoteza virutubisho pindi zinapofunguliwa.


Post a Comment

Previous Post Next Post