Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imeendesha mafunzo maalum kwa wazalishaji wa mbolea wenye viwanda vya kati, vidogo na vidogo sana kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa mbolea bora nchini.
Mafunzo hayo yamefanyika tarehe 2–3 Machi, 2026 katika ukumbi wa Edema mjini Morogoro, yakilenga kuwapatia wazalishaji uelewa katika maeneo mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa mbolea yenye ubora, kuzingatia viwango vinavyotakiwa pamoja na matumizi ya teknolojia sahihi ili kuzalisha bidhaa zenye tija kwa wakulima.
Wataalam kutoka taasisi mbalimbali walitoa mada katika mafunzo hayo ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Tanzania (SIDO), Taasisi ya Uhandisi na Ubunifu wa Teknolojia Tanzania (TEMDO) pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Aidha, washiriki walipata fursa ya kujifunza kuhusu upatikanaji wa mitaji na huduma za kifedha kupitia taasisi isiyo ya kiserikali ya Private Agricultural Sector Support (PASS), inayolenga kuwezesha uwekezaji katika sekta ya kilimo.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na wazalishaji wa mbolea kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Iringa, Geita, Mwanza, Simiyu na Dodoma.
Aidha, mafunzo kama haya yataendelea kufanyika tarehe 5 na 6 Machi, 2026 jijini Arusha, yakitarajiwa kuwahusisha wazalishaji wa mbolea kutoka mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Singida na Manyara, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uzalishaji wa mbolea bora nchini.
