SERIKALI YAENDELEA KUJIDHATITI UDHIBITI WA MAGONJWA ADIMU

 

Na Hassan Kimweri, WAF – Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika Sekta ya Afya, inaendelea kujidhatiti kwa kuimarisha mifumo ya huduma za afya kupitia tafiti mbalimbali ili kuhakikisha wagonjwa wenye magonjwa adimu wanapata huduma stahiki kwa wakati. 

Hayo yamesemwa leo Machi 4, 2026 na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe wakati akifungua Kongamano la 16 la kusambaza matokeo ya tafiti za magonjwa adimu lililofanyika Muhimbili University of Health and Allied Sciences (MUHAS) jijini Dar es Salaam. 

“Serikali inayapa uzito stahiki magonjwa haya adimu, ili tuweze kuyashughulikia kwa kina na upana wake, kwa kushirikiana na Taasisi kama Ali Kimara, sekta mashirika na sekta binafsi tutawafikia watoto wengi zaidi,” amesema Dkt. Magembe.

Aidha, Dkt. Magembe amesema hadi kufikia Desemba mwaka 2025 zaidi ya wataalamu wa afya 200 katika vituo 14 walikuwa wamepatiwa mafunzo ya kuanzisha vitengo vya tiba ya magonjwa adimu ikiwemo ‘hemofilia’ kuanzia ngazi ya msingi. 

“Serikali imeshachukua hatua za kujenga uwezo wa maabara yetu ya Taifa, mafunzo kwa wataalamu wa Afya na kuanzisha vitengo maalum vya matibabu ya magonjwa adimu kuanzia ngazi ya msingi (Zahanati, kituo cha afya na hospitali za wilaya), tulianza na Seli mundu (Sickle cell) na sasa Hemofilia ambapo tayari wagonjwa 500 wamegundulika na wanaendelea na tiba,” amesema Dkt. Magembe.

Pia, katika Kongamano hilo Dkt. Magembe amewataka wataalamu hao wa tafiti wakiwemo MUHAS na NIMR kujadilina kwa kina na kwa uwazi kujua mafaniko, changamoto na kutoa mapendekezo na kuyawasilisha Serikalini yaweze kufanyiwa kazi. 

Kongamano hilo limeandaliwa na Muhimbili University of Health and Allied Sciences (MUHAS) kwa kushirikiana na Taasisi ya Ali Kimara Rare Disease Foundation (AKRDF).        

Post a Comment

Previous Post Next Post