TANZANIA YAENDELEA KUIMARISHA HATUA ZA KUPAMBANA NA UKATILI WA KIJINSIA

 

Na WMJJWM – New York, Marekani

 

Serikali ya Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kutekeleza kikamilifu makubaliano ya kimataifa yanayohusu usawa wa kijinsia na maendeleo, sambamba na kuimarisha juhudi za kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.

 

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema Tanzania inaendelea kuthibitisha dhamira yake ya kutekeleza kikamilifu na kwa ufanisi hatua zilizowekwa katika makubaliano mbalimbali ya kimataifa kuhusu jinsia na maendeleo ambayo nchi imeridhia.

Dkt. Gwajima amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoingia katika makubaliano na maazimio mbalimbali ya kimataifa, ikiwemo Azimio na Jukwaa la Utekelezaji la Beijing, Mkataba wa Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW) pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030.

 

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali yenye lengo la kuhakikisha vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia vinatokomezwa katika maisha ya umma. Miongoni mwa hatua hizo ni utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (NPA-VAWC) wa mwaka 2024/25 hadi 2028/29, unaolenga kupunguza vitendo vya ukatili kwa asilimia 50.

“Kupitia mpango huo, Serikali imeendelea kupanua dawati za jinsia na watoto katika vituo vya polisi, ambapo zaidi ya dawati 420 yameanzishwa nchini kote. Pia imeanzisha vituo jumuishi vya huduma (One Stop Centres) katika baadhi ya vituo vya afya ili kutoa msaada wa kitabibu na kisheria kwa waathirika wa ukatili,” amesema Dkt. Gwajima.

 

Ameongeza kuwa katika kupambana na vitendo hivyo, Serikali imeendelea kutekeleza sheria mbalimbali zinazolinda haki za wanawake na watoto, ikiwemo Sheria ya Mtoto. Aidha, imeendelea kuimarisha kampeni na programu za kupambana na vitendo vya ukeketaji pamoja na ndoa za utotoni.

 

Dkt. Gwajima pia amefafanua kuwa kutungwa kwa Sheria ya Msaada wa Kisheria Na. 1 ya mwaka 2017 kumewezesha kupanua huduma za msaada wa kisheria kwa makundi yaliyo katika mazingira magumu, hususan wanawake maskini wa vijijini, wajane na watu wenye ulemavu.

 

“Serikali pia imefanya marekebisho katika Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Criminal Procedure Act) kwa kuweka masharti makali zaidi, ikiwemo kuwanyima dhamana watuhumiwa wa makosa ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, pamoja na kuongeza adhabu zinazoweza kutolewa na mahakama kwa makosa hayo,” amesisitiza Dkt. Gwajima.

 

Katika kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji, amesema Tanzania imeanza kutumia teknolojia za kidijitali katika kuchora ramani ya matukio ya ukatili wa kijinsia, sambamba na kuongeza uwezo wa vyombo vya dola na watendaji wa sekta ya sheria kupitia mafunzo maalum.

 

Kwa upande wa jamii, Serikali imeendelea kuhamasisha ushiriki wa wanaume na vijana wa kiume katika kubadili mitazamo na mila potofu zinazoendeleza ukosefu wa usawa wa kijinsia. Juhudi hizo zinafanyika kupitia kampeni mbalimbali za uhamasishaji, ikiwemo kampeni ya kimataifa ya “Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia.”

 

Amesema pamoja na kuwepo kwa changamoto kadhaa, Tanzania itaendelea kujenga juu ya mafanikio yaliyopatikana kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo sekta binafsi na asasi za kiraia, ili kusimamia na kupanua utekelezaji wa ahadi za kitaifa, kikanda na kimataifa katika kukuza usawa wa kijinsia na kulinda haki za wanawake na watoto

Post a Comment

Previous Post Next Post