Mwandishi Wetu,
Maafisa kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) wametoa elimu kwa wakulima na wanafunzi wa Shule ya Msingi Katawa katika Kijiji cha Kantawa, Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya mbolea ili kulinda afya ya udongo na kuongeza uzalishaji wa mazao.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Udhibiti Ubora wa TFRA, Henerico Renatus, alisema matumizi yasiyo sahihi ya mbolea, hasa mbolea za chumvi chumvi, yanaweza kuharibu udongo na kusababisha kupungua kwa tija ya mazao kwa wakulima.
Wakulima pia walipatiwa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea za ruzuku na umuhimu wa kupima afya ya udongo kabla ya kutumia mbolea ili kupata matokeo bora.
Kwa upande wao, wakulima walishukuru Serikali kwa mpango wa ruzuku ya mbolea ambao umewasaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kupelekea kuongeza ukubwa wa mashamba wanayolima.




