KAMATI YA BUNGE YAMPA TANO RAIS SAMIA KWA MAKUMBUSHO YA JIOPAKI YA NGORONGORO LENGAI


 

Na Sixmund Begashe, Karatu

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imetaka Makumbusho mpya ya Urithi Jiopaki iliyopo katika mradi wa Jiopaki ya Ngorongoro Lengai Wilayani Karatu kutumika kama zao jipya la utalii litakaloongeza idadi ya siku kwa wageni wanaotembelea vivutio vya utalii hapa nchini.

Maelekezo hayo yametolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) mara baada ya Kamati hiyo kutembelea na kukagua makumbusho hiyo iliyojengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya watu wa China.

Mhe. Mnzava amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa Makumbusho hiyo ya kisasa iliyogharimu shilingi Bilioni 20 na kwamba makumbusho si tu ni zao jipya la utalii bali ni muhimu kwa uhifadhi wa historia adhimu ya binadamu.

Mhe. Mnzava ameongeza kuwa, licha ya kuipongeza Serikali kwa mradi huo, pia Kamati yake imeridhishwa na ubora wa ujenzi jengo linalo dhihirisha uwepo wa thamani halisi ya fedha.

Aidha ameielekeza Wizara hiyo, kuhakikisha inaitangaza vyema Makumbusho hiyo ili kuvutia watalii wengi zaidi katika eneo hilo na nchini kwa ujumla.

Naye Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameishukuru Kamati hiyo kwa kutembelea Makumbusho hiyo huku akiahidi kusimamia kikamilifu utekelezaji wa maoni yote yaliyotolewa na waheshimiwa wajumbe

Ziara hiyo katika Makumbusho iliyosheheni utajiri mkubwa wa urithi wa jiolojia, historia ya Chimbuko la Mwanadamu na utamaduni wa jamii zinazopatikana katika eneo la jiopaki , imehudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Mhe. Dkt. Lameck Karanga, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Nkoba Mabula, baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Wizara na wataalam mbalimbali wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Post a Comment

Previous Post Next Post