
HOSPITALI ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC), inayosimamiwa na Taasisi ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), inatarajia kufanya kambi maalum ya siku tano ya uchunguzi wa magonjwa ya mifupa na mishipa ya fahamu bila malipo.
Kambi hiyo itafanyika kuanzia Februari 23 hadi 27, 2026 katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC), mkoani Arusha, ikiwa na lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwapatia huduma za kibingwa karibu na maeneo yao.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI katika hospitali hiyo, Dk. Tatizo Waane, amesema kuwa madaktari bingwa watano watashiriki katika kambi hiyo, huku wakitarajia kuhudumia wagonjwa takribani 200 kwa siku.
“Tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kupatiwa uchunguzi na ushauri wa kitaalamu kuhusu afya zao. Tumejipanga kuhakikisha huduma zinapatikana kwa ufanisi,” amesema Dk Waane.
Ameongeza kuwa bado kuna changamoto kubwa ya magonjwa ya moyo inayochangiwa na mtindo usiofaa wa maisha, ikiwemo uvutaji sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi na lishe isiyo sahihi.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa Mbobezi wa Mifupa na Uti wa Mgongo na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Anthony Assey, amesema ongezeko la uzito kwa wananchi wengi limechangia kuongezeka kwa maumivu ya viungo.
“Zamani watu walikuwa wakitembea kwa miguu na kujishughulisha na kazi za mikono, hali iliyosaidia kuupa mwili mazoezi ya kutosha. Sasa wengi wanatumia magari, bajaji na bodaboda, hali inayopunguza shughuli za mwili,” amesema Dk Assey.
Ameeleza kuwa matumizi ya pombe, tumbaku na kutofanya mazoezi ni miongoni mwa sababu zinazopelekea maumivu ya magoti, nyonga na mgongo pamoja na magonjwa mengine ya mifupa na viungo.
Wataalamu hao wamewashauri Watanzania kuzingatia lishe bora, kupunguza matumizi ya vilevi na kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa ya moyo na maumivu ya viungo.
Huduma hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Samia Suluhu Hassan, ambaye amesisitiza umuhimu wa kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi ili kuwapa fursa ya kupata uchunguzi na matibabu kwa urahisi.
Wananchi wa Arusha na maeneo jirani wametakiwa kutumia fursa hiyo muhimu kwa ajili ya kuchunguza afya zao na kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa madaktari bingwa.