
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, akizungumza Februari 27, 2026 jijini Dodoma wakati akizindua Vikundi Kazi 8 vya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II).
Na. Meleka Kulwa- Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ameonya juu ya kampeni na matangazo yanayohusisha masuala ya ushoga na usagaji na kusema kuwa hayakubaliki katika jamii kwa kuwa yanakwenda kinyume na mila na desturi za taifa. Amesema kuwa ni muhimu kuimarisha kanuni na sheria ili kukabiliana na vitendo vinavyokiuka maadili na kuhakikisha ulinzi wa watoto na wananchi wote.
Ameyasema hayo wakati wa Uzinduzi wa Vikundi Kazi 8 vya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II), Februari 27, 2026, jijini Dodoma.
Ameongeza kuwa vikundi kazi vilivyozinduliwa vitasaidia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II) kupitia elimu kwa jamii na uratibu wa juhudi za kupunguza ukatili. Aidha amebainisha kuwa mafanikio ya mpango huo yanategemea ushirikiano wa wadau na taasisi mbalimbali katika kuchukua hatua zinazolinda makundi yaliyo hatarini.
Naye, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii na Makundi Maalum,Wakili Amon Mpanju, amesema kuwa mafanikio ya MTAKUWWA yatategemea ushirikiano wa sekta zote na jamii. Aidha amebainisha kuwa kamati za ulinzi wa wanawake na watoto zinapaswa kuimarishwa ili kuchukua hatua dhidi ya ukatili na kutoa taarifa zitakazosaidia kuboresha ulinzi wa makundi yaliyo hatarini.
Awali, Mkurugenzi wa Shirika la Kivulini, Yasin Ali, amesema kuwa juhudi za serikali pamoja na wadau zimechangia kupungua kwa ukatili katika mikoa ya Kanda ya Ziwa. Ameongeza kuwa takwimu zinaonyesha Mkoa wa Mara umeshuka kutoka asilimia 78 hadi 66, Shinyanga kutoka 78 hadi 68, Mwanza kutoka 60 hadi 47, Kigoma kutoka 61 hadi 34, na Geita kutoka 63 hadi 42, ishara ya mafanikio yanayotokana na ushirikiano wa Serikali na wadau.
Vikundi hivyo vitajikita katika kuimarisha uchumi wa kaya, mila na desturi, na mazingira salama katika jamii. Pia vitatumia vyombo vya habari na TEHAMA kuelimisha, kuboresha malezi na huduma kwa manusura wa ukatili, pamoja na kusimamia utekelezaji wa sheria. Uzinduzi huo unalenga kuongeza uratibu na uwajibikaji, kuimarisha ushirikiano wa wadau, na kufuatilia matokeo ya juhudi za kupambana na ukatili wa kijinsia.
