Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Adolph Mkenda afungua mlango wa mazungumzo kwa Taasisi na Makampuni mbalimbali kuunga mkono juhudi za Rais Dkt Samia kusomesha Wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo ya Sayansi kutoka ngazi ya awali ya kidato cha sita hadi ngazi ya Shahada ya Uzamili kwani Wizara imejipanga vizuri kuhakikisha fedha watakazotoa zinakwenda mahali panapotakiwa
Waziri Mkenda ameyasema hayo leo Jijini Dodoma Februari 25,2026 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu kutolewa kwa ufadhili huo na Wanafunzi kuripoti katika Vyuo husika.
Ambapo amesema kuwa tayari walishapanga kutoa ufadhili katika ngazi ya Shahada ya Uzamili na kwa kuanza waliamua kupeleka Wanafunzi katika Vyuo viwili vya hapa nchini cha Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Arusha na kampasi ya Indian Institute of Teknoloji kilichopo Zanzibar ambavyo vyote vimejikita katika masuala ya Sayansi.
Na kuongeza kuwa tayari Wanafunzi wamesharipoti katika Chuo cha Nelson Mandela na kuanza masomo kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili na kwa awamu ya pili watawapeleka wengine tena 10 katika kampasi ya Indian Institute of Teknoloji kwaajili ya kusoma mambo ya Data Science,Akili unde na mambo mengine ya kisayansi ili kuendana na kasi ya Dunia katika Sayansi na Teknolojia.
"Kwahiyo napenda nitoe kauli hii kwa Benki,Migodi,Taasisi na Mashirika mbalimbali ambayo yanapenda kuunga mkono juhudi za Rais wetu za kusomesha tukae tuongee na tutakuwa na mkutano wa kuzungumza pamoja na kuwahakikishia tutakavyogawa nafasi bila bila kona kona ili hela mtakazoleta ziende mahali panapotakiwa".
Aidha amesema kuwa kwa mwaka huu wameanza kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa kupeleka vijana waliofanya vizuri kwenda kusoma masuala ya Data Science, Akili unde na mambo mengine ya kisayansi ambapo tayari wameshapeleka wanafunzi 16 huko Johannesburg Afrika ya Kusini na wameanza masomo kwa ufadhili huo.
Ambapo pia wanafunzi wengine 34 wanatajiwa kuondoka kati ya mwezi wa 8 au 9 kwenda Iland kwaajili ya masomo hayo hayo ya Sayansi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Tume ya Sayansi na Teknolojia ambao ndio waratibu wa Program hiyo ya Samia Scholarship Extended Dkt Amos Nungu amesema kuwa wameona muitikio mkubwa kwa watoto na thamani ambayo watoto wameipa program hiyo,na kuamini kuwa idadi itaongezeka kwa wakati mwingine, zaidi ya hawa walioenda katika awamu hii.
Naye Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Arusha ambao ndio watekelezaji wa programu hii Prof Maulilio Kipanyula amesema Taasisi hiyo haikuchaguliwa kwa bahati mbaya kwasababu Wanafunzi wanaokwenda pale wanapata kuchanganyikana na wanafunzi kutoka Mataifa mengine kwani asilimia 10 ya wanafunzi wao ni wa Kimataifa hivyo wanapata uzoefu kupitia kukutana kwao na kuwa pamoja.





