
Sekta ya Madini Tanzania kupitia Kongamano la Mining Indaba 2026 imeendelea kuimarisha nafasi yake kimataifa, huku Tanzania ikiendelea kujidhihirisha kama kimbilio la uwekezaji katika Sekta ya Madini kwa kuvutia mashirika ya kimataifa, kampuni mbalimbali na wawakilishi wa kidiplomasia.
Februari 10, 2026, Waziri wa Madini alikutana na wadau muhimu ikiwemo Benki ya Dunia katika vikao vya pembeni vya kongamano linaloendelea jijini Cape Town, Afrika Kusini, pamoja na kushiriki Mkutano wa Mawaziri wa Madini wa SADC.
Katika kikao kilichofanyika baina ya ujumbe wa Australia na Tanzania, Naibu Balozi wa Australia Christopher Ellinger alieleza kuvutiwa na mwenendo wa Sekta ya Madini nchini na kusema kwamba kwa kampuni za Australia, Tanzania ni moja ya machaguo ya kwanza kwa uwekezaji. Pia, amesisitiza utayari wa nchi hiyo kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza miradi ya madini kupitia kampuni za Australia, na kuomba ufafanuzi wa Kanuni za Madini za ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta, hasa katika utoaji wa huduma migodini.
Benki ya Dunia imetambua sekta ya madini Tanzania kama eneo la kimkakati lisilopaswa kuachwa pembeni katika juhudi za maendeleo na uwekezaji, ikiashiria uhitaji wa kuendelea kuwekeza na kushirikiana na serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuongeza faida za kiuchumi.
Benki hiyo imeunga mkono mpango wa Tanzania kujiimarisha katika shughuli za utafutaji na utafiti wa rasilimali madini na dhamira ya uongezaji thamani madini ndani ya nchi badala ya kutegemea uzalishaji na usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi. Hii inaonesha umuhimu wa sekta ya madini katika mipango ya maendeleo ya Tanzania na uhusiano wake na wadau wa kimataifa.
Waziri wa Madini alisisitiza dhamira ya Serikali kuimarisha ushirikiano wa kufanya tafiti za kina za jiosayansi ambazo zitaongeza wingi wa taarifa na kuchochea uwekezaji nchini. Aidha, Waziri Mavunde amesisitiza umuhimu wa kipaumbele cha kuongeza thamani madini ndani ya nchi kama njia ya kuongeza manufaa yatokanayo na rasilimali madini badala ya kuuza madini ghafi kwa waongezaji thamani nje ya nchi.
Waziri wa Madini Anthony Mavunde alisisitiza kwamba kaulimbiu ya “Madini ni Maisha na Utajiri” inaweka kipaumbele cha kufanya tafiti za jiosayansi na kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi. Amesema Serikali iko tayari kushirikiana na wawekezaji wote wanaochangia maendeleo ya sekta ya madini nchini kwa kuzingatia Kanuni, Sheria na miongozo iliyowekwa.
Aliyasema hayo alipokutana na Kampuni ya Faru Graphite inayomilikiwa kwa ubia baina ya Serikali na Kampuni ya Black Rock Mining inayotarajia kuchimba madini ya kinywe katika eneo la Mahenge, Wilayani Ulanga, Mkoani Morogoro. Katika kikao hicho, kampuni hiyo imetangaza maendeleo mazuri kwenye mradi huo na kuwashukuru viongozi wa Serikali kwa ushirikiano unaowawezesha kufanikisha kazi.
Katika kikao na Waziri Mavunde, kampuni ya uchimbaji madini na ukodishaji wa vifaa vya uchimbaji ya Plantcor Mining yenye makazi yake nchini Afrika Kusini, ambayo ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kusaini Mkataba na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), ilimhakikishia kuwa mara baada ya kusaini mkataba huo wa ubia itaanza kushirikiana na STAMICO kuendeleza mradi wa uchimbaji madini ya dhahabu kwenye leseni inayomilikiwa na STAMICO katika eneo la Kigosi, Mkoani Geita.
Kampuni ya Breakthrough Attorneys na Benki ya NMB zimeshirikiana kuandaa na kutekeleza warsha ya kuitangaza sekta ya madini na kuvutia uwekezaji nchini Tanzania. Warsha hiyo ilifanyika Februari 10, 2026 jijini Cape Town, Afrika Kusini, na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya madini kutoka sehemu mbalimbali duniani. Breakthrough Attorneys ni kampuni ya kisasa ya huduma za kisheria yenye makao yake Tanzania inayotoa huduma za kimataifa kwa kampuni, taasisi za fedha, taasisi za Serikali na watu binafsi.
Akizungumza katika warsha hiyo, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde ambaye alikuwa mgeni rasmi, alieleza kuwa Tanzania inahama kutoka kumiliki rasilimali za madini pekee kwenda kushiriki kikamilifu katika mnyororo mzima wa thamani wa madini. Alisisitiza kuwa uongezaji thamani nchini Tanzania si kikwazo bali ni fursa, na kuwaasa wawekezaji kuitumia kikamilifu.
Alisema kuwa uongezaji thamani madini unaodhamiriwa Tanzania ni ule unaojengwa kupitia ushirikiano unaoendana na Dira ya Madini ya Afrika (Africa Mining Vision) na sera za viwanda rafiki kwa wawekezaji.
Mhe. Mavunde alipongeza ongezeko la mchango wa taasisi za fedha nchini, akitolea mfano wa Benki ya NMB ambayo inashirikiana kikamilifu na wawekezaji wa madini katika hatua zote za mnyororo wa thamani na kushiriki kuvutia wawekezaji ndani na nje ya nchi.
“Muunganiko kati ya ufadhili wa kifedha wa ndani na wa kimataifa ni ishara muhimu inayoashiria kuwa sekta ya madini ya Tanzania ina uwezo wa kufadhiliwa, kukopesheka, na kuvutia uwekezaji,” alisema Waziri Mavunde.
