Naibu Kamshna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Mcha Hassan Mcha ameeleza kuwa TRA inaendelea kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) katika utekelezaji wa mradi wa kujenga uwezo wa kitaaluma kwa watumishi wake ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa kodi.
Ameyasema hayo tarehe 10.02.2026 katika kikao na wajumbe wa JICA wanaotekeleza mradi huo wa kuwajengea uwezo watumishi wa TRA ulioanza mwaka 2023 na unaotarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.
Bw. Mcha amesema lengo la mradi huo ni kuwajengea uwezo watumishi katika kubaini maeneo muhimu ya kufanyia uchunguzi wa kodi kwa kutumia mbinu za kitaalamu na uchambuzi wa takwimu.
Bw. Mcha amesema mradi huo unatekelezwa katika mikoa mitatu ya kikodi ambayo ni Kinondoni, Temeke na Arusha, huku matarajio yakiwa ni kuusambaza katika mikoa mingine.
Amebainisha kuwa tayari kuna mafanikio ya awali ambapo utekelezaji umeanza katika sekta ya ujenzi, huku mipango ikiendelea kuupanua katika sekta nyingine ikiwemo utalii na sekta nyingine muhimu za kiuchumi.
