MAJIKO BANIFU 6,000 KUSAMBAZWA SIMIYU

 

Mwandishi Wetu Simiyu,

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeanza kusambaza majiko banifu 6,236 katika Wilaya tano za Mkoa wa Simiyu, ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya nishati safi, salama na nafuu ya kupikia kwa Watanzania wote. 

Majiko hayo ambayo yanatolewa kwa wanachi kwa bei ya ruzuku, yanasambazwa na Kampuni ya Geita Millenium Star Ltd, ambapo kila wilaya itapata majiko 1,247 ambayo yatagawiwa kwa wananchi.

Akizungumza mara baada ya kupokea majiko hayo Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Faiza Salim ameishukuru Wizara ya Nishati kupitia REA, kwa kuleta majiko hayo kwa bei ya ruzuku.

Mhe. Faiza amesisitiza majiko hayo kupelekwa zaidi katika kata zilizopo pembezoni ambazo hazikufikiwa na zoezi la usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia LPG. 

“ Tatizo kubwa la ukataji wa miti ovyo, kuharibu mazingira lipo maeneo ya vijijini, haswa maeneo ambayo bado hayajafikiwa na vyanzo vingine vya nishati ya kupikia, hivyo niwaombe majiko haya yapelekwe kwa kasi uko vijijini kwani uharibifu mkubwa upo huko, ” Amesema Mhe. Salim. 

Naye, Mhandisi wa Miradi kutoka REA Geofrey Gedo amesema Serikali imetenga takribani Shilingi Milioni 218 kusambaza majiko banifu ndani ya Mkoa wa Simiyu.

Mhandisi Gedo ameongeza kuwa gharama halisi ya majiko banifu yanauzwa kwa Shilingi 35,000 ambapo wananchi wamepunguziwa gharama hiyo na Serikali kupitia ruzuku ya asilimia 85, na hivyo kupelekea zaidi ya robo tatu ya gharama halisi kubebwa na Serikaki.

“Kupitia ruzuku hiyo, wananchi wanapatiwa majiko hayo kwa bei ya Shilingi 5,250 na Serikali inachangia kiasi cha Shilingi 29,750 sawa na asilimia 85 ya bei halisi ya jiko banifu, lengo la Mhe. Rais Samia ni kuhakikisha wananchi wenye kipato cha chini wa wanaweza kununua majiko haya,” Amesema Mha. Gedo.

Kwa upande wake, Meneja Usambazaji kutoka Kampuni inayozalisha majiko hayo ya Geita Millenium Hamis Kashilila amesema kuwa majiko hayo ni bora na yamepimwa na mamlaka ya kudhibitisha ubora wa majiko nchini TILDO.

Ameongeza kuwa majiko hayo yametengezwa kitaalamu hasa katika eneo la kuzingatia afya za wananchi, kwani yana uwezo na kiwango kikubwa cha kupunguza hewa chafu ya ukaa. 

Aidha Meneja huyo amesema kuwa majiko hayo yanatumia mkaa mchache, ambapo gunia moja la mkaa ambalo lilikuwa linatumika kwa mwezi mmoja kwa majiko ya kawaida katika majiko hayo banifu linatumika kwa muda wa miezi miwili.

Baadhi ya wananchi ambao walipokea majiko na wengine ambao wameanza kuyatumia katika Kata ya Lamadi wamemshukuru Rais Samia pamoja na REA kwa kuwaletea majiko hayo ambayo yana bei nafuu.

“ Mimi nimechukua jana kwa bei ya Sh 5,250 majiko haya ni mazuri sana, wananchi wanaohitaji ni wengi sana hapa tunaona yaliyoletwa ni machache sana, tunamuomba Rais wetu Dkt. Samia atuongezee haya ni machache sana,” Alisema Yohana Renatus.

Naye Bitishiba Makulu mkazi wa Kata ya Lamadi alimshukuru Rais Dkt Samia kwa kuwapatia majiko hayo kwa bei ya Ruzuku, ambapo alisema kuwa bei hiyo ni ndogo sana na kila mtanzania anao uwezo wa kuimudu.   

Post a Comment

Previous Post Next Post