
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari, amekutana na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Usimamizi wa Anga Duniani (ICAO) Bw. Michael Gill na kufanya mazungumzo tarehe 26 Februari, 2026 katika Ofisi ndogo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dar es salaam.
Aidha Mhe. Johari alimshukuru Mkurugenzi wa ICAO kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa mafunzo hayo, akibainisha kuwa kupitia mafunzo hayo Mawakili wa Serikali wanapata fursa ya kujifunza na kuimarisha uelewa wa Sheria za anga na mikataba ya kimataifa.
Vile vile Mhe. Johari ameeleza kuwa Serikali ipo katika hatua za kupitia mikataba ya kimataifa inayohusu sekta ya anga ili kukamisha uridhiwaji kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa ICAO Bw. Michael Gill alimshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa warsha iliyoandaliwa kwa pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Anga Tanzania (TCAA) na Shirika la Kimataifa la Usimamizi wa Anga Duniani (ICAO), inayolenga kujenga uwezo wa kitaalamu na kuimarisha utekelezaji wa viwango vya kimataifa vya usalama wa anga.
Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Usimamizi wa Anga Duniani (ICAO) Bw. Michael Gill aliambatana na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Salim Msangi, Mkuu wa Kitengo cha Sheria TCAA Bi. Maria Memba Pamoja na Afisa Sheria wa ICAO Bw. Andrew Opolot.