Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi zawadi Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi hiyo Dkt. Hassan Mahmoud Mshinda alipotembelea JKCI kwa mara ya kwanza leo kwaajili ya kuona utendaji kazi pamoja na kukutana na viongozi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimweleza utendaji kazi wa taasisi hiyo Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wadhamini ya JKCI Dkt. Hassan Mahmoud Mshinda alipotembelea taasisi hiyo kwa mara ya kwanza leo kwaajili ya kuona utendaji kazi pamoja na kukutana na viongozi.
Baadhi ya viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimsikiza Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wadhamini ya JKCI Dkt. Hassan Mahmoud Mshinda alipotembelea taasisi hiyo kwa mara ya kwanza leo kwaajili ya kuona utendaji kazi pamoja na kukutana na viongozi.
***************************************************************************************************************************************************************************************************
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wadhamini ya taasisi hiyo, Dkt. Hassan Mahmoud Mshinda wakati wa ziara yake ya kwanza JKCI kwaajili ya kuona utendaji kazi pamoja na kukutana na viongozi wa taasisi hiyo.
Dkt. Mshinda alisema ameridhishwa na kasi ya maendeleo, ubunifu na uthubutu uliofanywa na taasisi hiyo katika kuboresha huduma za moyo nchini.
“Nimejionea kwa macho yangu ubora wa huduma na mipango mikubwa ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa. Si rahisi kwa taasisi nyingi kuwa na ujasiri wa kujaribu na kuwekeza katika teknolojia za kisasa kama ilivyofanywa hapa, haya ni mafanikio yanayostahili pongezi,” alisema Dkt. Mshinda.
Alisisitiza kuwa Bodi ya Wadhamini itatoa ushirikiano wa karibu kwa uongozi wa taasisi hiyo ili kuhakikisha malengo ya kuimarisha huduma za moyo yanatimia kwa ufanisi na kwa manufaa ya Watanzania wote.
Akigusia uzoefu wake binafsi, Dkt. Mshinda alisema aliwahi kupatiwa matibabu katika taasisi hiyo na kushuhudia viwango vya juu vya huduma vinavyolingana na vya mataifa yaliyoendelea.
“Nimewahi kutibiwa hapa. Naweza kusema bila kusita kuwa huduma za hapa na za Switzerland hazina tofauti kubwa. Hata wenzetu wa huko walishangaa kusikia kuwa Tanzania ina taasisi ya kiwango hiki”, aliongeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge alisema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza rufaa za wagonjwa wa moyo waliokuwa wakipelekwa nje ya nchi kwa matibabu maalum jambo lililookoa fedha nyingi za Serikali na kupunguza adha kwa wagonjwa na familia zao.
Alifafanua kuwa taasisi hiyo imepanua wigo wa huduma kwa kuanzisha matawi sita katika maeneo mbalimbali ya nchi, hatua iliyosaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika makao makuu na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.
“Mbali na huduma za ana kwa ana, tumeanza pia kutoa huduma kwa njia ya mtandao hususan kwa wagonjwa wa shinikizo la damu ili kurahisisha ufuatiliaji wa matibabu na kupunguza gharama na muda wa safari”, alisema Dkt. Kisenge.
Alibainisha kuwa JKCI ni miongoni mwa taasisi chache barani Afrika zenye uwezo wa kufanya upasuaji wa moyo kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya tundu dogo, pamoja na kumiliki mtambo wa Carto 3 kwaajili ya matibabu ya umeme wa moyo ambao ni wa kipekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Dkt. Kisenge alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan,kwa kuendelea kuiunga mkono taasisi hiyo na kwa kumteua Dkt. Mshinda kuiongoza Bodi ya Wadhamini huku akieleza akieleza kuwa uzoefu wake katika utafiti utaongeza nguvu katika eneo la tafiti za magonjwa ya moyo.
Katika ziara hiyo Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wadhamini ya JKCI alitembelea pia JKCI Hospitali ya Dar Group ambapo Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Dkt. Tulizo Shemu, alisema tangu hospitali hiyo ilipokabidhiwa kwa JKCI mwishoni mwa mwaka 2022 imefanya maboresho makubwa ya miundombinu na utoaji wa huduma.
Dkt. Shemu alieleza kuwa idadi ya wagonjwa wa nje imeongezeka kutoka wastani wa 200 hadi kufikia 650 pia wamefanya ujenzi wa chumba cha kisasa cha upasuaji, wameboresho eneo la OPD, ujenzi wa jengo la VIP, pamoja na ongezeko la vifaa tiba na uwepo wa wataalamu mabingwa wa magonjwa mbalimbali.
Dkt. Shemu alisema Hospitali ya Dar Group inatoa huduma za matibabu ya magonjwa mbalimbali ikiwemo matibabu za moyo, huduma za upasuaji, matibabu ya magonjwa ya wanawake na watoto, matibabu ya afya ya kinywa na meno, matibabu ya macho, huduma za mazoezi tiba, matibabu ya mifupa, pamoja na huduma za dharura.
“Hospitali ya Dar Group ilianzishwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kupitia azimio maalumu la mwaka 1981 na kusajiliwa na Wakala wa usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) mwaka 1997 chini ya sheria ya makampuni ya mwaka 1967 ikihusishwa na dhamana isiyo mtaji”, alisema Dkt. Shemu.


