
Gavana wa Jimbo la Maniema, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mhe. Moise Kabwankubi ameongoza ujumbe kutoka nchi hiyo kuzuru Hospitali ya Taifa Muhimbili na taasisi zake ili kujionea utendaji kazi na kuangalia fursa za ushirikiano katika sekta ya afya.
Mhe. Kabwankubi na ujumbe wake wamezungumza na uongozi wa Muhimbili na kutembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) pamoja na Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI).
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge ameeleza kuwa Taasisi hiyo ipo tayari kusaini Hati ya Makubaliano na DRC ili kuweza kusaidia wagonjwa wengi zaidi kutoka DRC kupata matibabu lakini pia wapo tayari kufungua tawi lake nchini DRC.
Akiwa Muhimbili, Mhe. Kabwankubi amepongeza jitihada na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Tanzania kwenye sekta ya afya na kuonesha shauku ya kujua zaidi nini siri ya mafanikio kwa Tanzania kuwa na taasisi kubwa za afya zenye ufanisi wa hali ya juu.
Ameomba ushirikiano kati ya Tanzania na DRC katika sekta ya afya uweze kupanuka zaidi kupitia kubadilishana ujuzi na uzoefu wa kujenga na kuendesha taasisi kubwa kama hizi kwa weledi na ufanisi ili kuweza kutoa huduma zilizo bora kwa wananchi wengi wa DRC.
