Waziri Mavunde Apongeza Ushirikiano Benki Ya CRDB na Tume ya Madini Uwezeshaji Wachimbaji Wadogo wa Madini

 

Dar es Salaam, 23 Februari 2026 — Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amepongeza kwa ushirikiano wa kimkakati kati ya Benki ya CRDB na Tume ya Madini, akieleza kuwa mpango maalum wa kifedha uliozinduliwa leo kwa ajili ya wachimbaji wadogo ni hatua ya kihistoria itakayobadili kabisa mfumo wa upatikanaji wa mitaji katika sekta ya madini nchini.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa huduma hizo na utiaji saini wa Mkataba wa Makubaliano (MOU) uliofanyika katika hoteli ya Johari Rotana, Waziri Mavunde alisema sekta ya madini imeendelea kukua kwa kasi, ikichangia asilimia 10 ya Pato la Taifa na zaidi ya asilimia 56 ya mapato ya fedha za kigeni kupitia mauzo ya nje yanayozidi dola za Marekani bilioni 5 kwa mwaka.
“Sekta ya madini sasa ni injini ya uchumi wetu. Tunachokishuhudia leo ni daraja linalounganisha maono ya Serikali na nguvu ya mtaji kutoka sekta ya fedha. Ushirikiano huu unaenda moja kwa moja kumgusa mchimbaji mdogo na kumwinua katika uchumi rasmi. Benki ya CRDB hakika mmeonyesha kuwa ni Benki kiongozi katika kuleta suluhisho stahiki kwa sekta mbalimbali. Tunawashukuru sana,” alisema Waziri Mavunde.

Alisisitiza kuwa chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imekuwa ikitekeleza mageuzi ya kisera, kiusimamizi na kisheria ili kuhakikisha sekta ya madini inawanufaisha Watanzania wengi zaidi, hususan wachimbaji wadogo. Alieleza kuwa azma ya Serikali ni kuona uchimbaji hauishii kwenye kuuza mawe ghafi, bali unapanuka hadi kwenye uchakataji na uongezaji thamani ndani ya nchi.
Mpango uliozinduliwa na Benki ya CRDB unaleta mageuzi makubwa katika mfumo wa dhamana kwa kutambua dhamana mbadala zinazotokana moja kwa moja na shughuli za uchimbaji. Kwa mara ya kwanza katika sekta ya benki nchini, leseni halali za uchimbaji, mikataba ya mauzo ya dhahabu, na akiba ya dhahabu iliyohifadhiwa katika viwanda vya kusafisha pamoja inatambuliwa kama dhamana zinazokubalika kwa ajili ya mikopo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema mpango huo ni mfumo kamili wa kifedha unaogusa mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya madini kuanzia uchimbaji, uchakataji, uhifadhi, usafirishaji hadi biashara na masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Huu ni muundo mpya wa kifedha unaotambua uhalisia wa sekta ya madini. Tumekubali dhamana zinazotokana na shughuli halisi za wachimbaji badala ya mali zisizohusiana na sekta.

 Hii itafungua milango kwa maelfu ya wachimbaji wadogo waliokuwa nje ya mfumo rasmi wa kifedha,” alisema Nsekela.
Alieleza kuwa mpango huo unajumuisha mikopo ya mtaji kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za uchimbaji, mikopo ya ununuzi wa mitambo na vifaa vya kisasa, mikopo inayodhaminiwa na dhahabu, huduma za bima za migodi na wafanyakazi kupitia CRDB Insurance, pamoja na akaunti maalum za miamala ya madini na dhahabu zitakazorahisisha ufuatiliaji na uwazi wa biashara.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi CRDB, Donald Mmari, alimweleza Waziri wa Madini kuwa Bodi imeweka miongozo ya kimkakati inayolenga kuhakikisha sekta ya madini inakua kwa kuzingatia misingi ya uendelevu, uwajibikaji na uchumi shirikishi.
“Tunataka kuona wachimbaji wadogo wanapanda ngazi kutoka uchimbaji wa jadi hadi kutumia teknolojia bora, kupata masoko rasmi na kushiriki katika uongezaji thamani. Ukuaji wa sekta ya madini lazima uwe endelevu na wenye manufaa kwa jamii,” alisema Dkt. Mmari.

Benki ya CRDB ni miongoni mwa taasisi chache za kifedha zilizowekeza kwa kiwango kikubwa zaidi katika sekta ya madini nchini. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, Benki hiyo imetoa mikopo yenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 186 katika sekta ya madini, ambapo shilingi bilioni 136 zimetolewa kwa wachimbaji wakubwa na shilingi bilioni 50 kwa wachimbaji wadogo.  

Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji, Rais wa Chama cha Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina alisema mpango huo umeleta matumaini mapya kwa wachimbaji wadogo waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya kukosa dhamana zinazokubalika na taasisi za fedha.
“Leo tunashuhudia mwanzo wa zama mpya. Wachimbaji wadogo tumepewa heshima ya kutambuliwa kama washirika halali wa maendeleo. Tunaishukuru sana Benki ya CRDB kwa kutuletea suluhisho hii, na tunawaahidi tutaendelea kushirikiana nao pamoja na Serikali kuhakikisha tunatumia fursa hii kwa uwajibikaji,” alisema.

Mkataba wa Makubaliano uliosainiwa kati ya Benki CRDB na Tume ya Madini unatarajiwa kuimarisha urasimishaji wa wachimbaji, kuongeza upatikanaji wa mitaji nafuu, kukuza ajira kwa vijana na wanawake katika maeneo ya migodi, pamoja na kuongeza mapato ya Serikali kupitia uwazi wa miamala na ufuatiliaji wa kidijitali.

Post a Comment

Previous Post Next Post