
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda Akizungumza wakati wa kikao kazi na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kilichofanyika Januari 20, 2025, Jijini Dodoma
Na. Meleka Kulwa
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa Serikali imejipanga kuimarisha mageuzi ya sekta ya elimu kwa kuzingatia matumizi sahihi ya takwimu, upanuzi wa fursa za masomo ya juu ndani na nje ya nchi, pamoja na utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka kumi.
Akizungumza wakati wa kikao cha nusu mwaka cha Menejimenti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara kilichofanyika January 20,2025, Jijini Dodoma, Prof. Mkenda amesema kuwa kikao hicho ni cha kimkakati kwa kuwa kinatoa nafasi ya kutathmini utekelezaji wa bajeti ya nusu mwaka na kupanga vipaumbele vya mwaka wa fedha unaofuata.
Pia, Amebainisha kuwa Serikali inalenga kutumia kikamilifu fursa za ufadhili wa masomo (scholarships) zinazotolewa na nchi na taasisi mbalimbali za kimataifa ili kupunguza utegemezi wa mikopo ya elimu ya juu na kutoa nafasi kwa Watanzania wengi zaidi kupata elimu.
Aidha amebainisha kuwa Tanzania imekuwa na changamoto ya kutotumia ipasavyo fursa nyingi za ufadhili zinazopatikana nje ya nchi kutokana na ukosefu wa taarifa, uratibu na mifumo thabiti ya ufuatiliaji. Amesisitiza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha fursa hizo zinawanufaisha Watanzania wengi zaidi.
Prof. Mkenda amesema kuwa Serikali ipo katika hatua za kuimarisha mfumo wa kitaifa wa takwimu za elimu ili kufuatilia mwenendo wa mwanafunzi tangu anapoanza elimu ya awali hadi elimu ya juu au mafunzo ya ufundi. Aidha amebainisha kuwa mfumo huo utawezesha Serikali kupata takwimu sahihi zitakazosaidia kupanga sera, bajeti na mipango ya maendeleo ya sekta ya elimu.
Aidha, Amesema kuwa uwepo wa takwimu zisizo sahihi au zisizounganishwa umekuwa changamoto katika kupanga sera na mipango ya muda mrefu, hivyo Wizara inalenga kuwa na mfumo mmoja unaosomana kati ya taasisi zote za elimu, ikiwemo Baraza la Mitihani (NECTA), NACTVET, vyuo vikuu na taasisi nyingine.
Amesema kuwa Serikali inaendelea na maandalizi ya utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka kumi, itakayohakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu hadi kidato cha nne bila kikwazo cha gharama. Aidha amebainisha kuwa utekelezaji wa mpango huo utahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Wizara, taasisi zake na wadau wa elimu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amesema kuwa kikao hicho ni fursa muhimu ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mwelekeo wa utekelezaji wa sera na mipango ya Wizara.
Aidha amebainisha kuwa Wizara itaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya viongozi wa Wizara, taasisi zake na wataalamu wa sekta ya elimu ili kuhakikisha mageuzi yanayopangwa yanatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa Taifa.
Akitoa maelezo ya awali ya kikao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa kikao cha nusu mwaka ni sehemu ya utaratibu wa Wizara wa kutathmini utekelezaji wa majukumu yake na kupanga kwa pamoja hatua za utekelezaji kwa kipindi kijacho.
Aidha amebainisha kuwa kikao hicho kinalenga kujadili utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo iliyoboreshwa, masuala ya elimu kidijitali, utekelezaji wa bajeti, pamoja na upatikanaji wa fursa za elimu na ufadhili wa elimu ya juu.
Pia, Amesema kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Wizara na Taasisi zilizo chini yake ni msingi muhimu wa kufanikisha dira ya maendeleo ya Taifa kupitia sekta ya elimu.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir Akizungumza wakati wa kikao kazi na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kilichofanyika Januari 20, 2025, Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo Akizungumza wakati wa kikao kazi na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kilichofanyika Januari 20, 2025, Jijini Dodoma.
